Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina

Search This Blog

Breaking

Serikali kuja na mpango wa kodi ya nyumba kulipwa mwezi mmoja mmoja

TANGAZA NASI HAPA


2016-02-10

Bomoabomoa yatua Bariadi nyumba 30 zabomolewa , baadhi walia, wengine wafurahi




Nyumba hizo zilizobolewa jana kuanzia saa 12.00 alfajiri kwa usimamizi wa maofisa wa Tanroads chini ya ulinzi wa askari wa jeshi la polisi mkoani hapa.
Baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo walidai kuwa hawakupewa muda wa kutosha kujiandaa kuondoa mali zao.
Reberata Mhagama alisema kabla ya ujenzi wa barabara ya Bariadi -Lamadi kwa kiwango cha lami, walifanyiwa tathmini na kuahidiwa kulipwa fidia.
“Nilifanyiwa tathmini mwaka 2012, tangu mwaka 1965 nipo eneo hili na nimekulia hapa. Awali barabara ilitakiwa kupita eneo la Malambo, lakini ikabadilishwa na kupita hapa,” alisema.
Mhagama alidai kuwa baada ya kufanyiwa tathimini ya nyumba yao na Serikali waliahidiwa kulipwa fidia ya Sh60 milioni ili waondoke kwenye eneo hilo.
Alidai anashangaa wamebomolewa nyumba hiyo bila ya kulipwa fidia hiyo na kupewa taarifa.
Baadhi ya wakazi walisema kubomolewa kwa nyumba hizo kumesababisha mji huo kuwa safi.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Bariadi, Othman Hamis alisema baadhi ya wamiliki hao walipewa muda wa kubomoa nyumba zao, lakini walikaidi.
“Tangu asubuhi tunakwenda vizuri, hawa wanaolia na kulalamika ni wale ambao walikaidi kubomoa nyumba zao wenyewe, walifikiri kuna utani kama ilivyozoeleka. Hapa ni Utekelezaji Tu,” alisema Hamis.
Meneja wa Tanrods wa Mkoa huo, Albert Kent alisema wamiliki hao walipewa notisi ya kuhama eneo hilo la barabara Julai 20, 2012 na kukimbilia Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kupinga.
Kent alisema katika kesi hiyo, Serikali ilishinda baada ya mahakama kusikiliza na kuamuru wamiliki hao kupewa notisi nyingine ya kuondoka eneo hilo Septemba 12, 2013 na kwenda kupinga tena mahakamani.
“Baada ya kupinga tena notisi hiyo kesi ilisikilizwa, kwa mara nyingine Serikali ilishinda na ilitolewa notisi mara ya tatu Aprili 28, 2014, lakini hawataki kutoka. Baada ya hali hiyo tumeamua kubomoa nyumba wenyewe,” alisema Kent.
Aliwalaumu wamiliki hao kwa kushindwa kutekeleza matakwa ya sheria na kukimbilia mahakamani.
“Walitakiwa kama hukumu imetoka na sisi tumewapa muda wa kuondoka, basi wangeondoka mara moja, lakini ukigoma ndiyo kama hivi Serikali itakubomolea ili kutekeleza sheria inavyotaka,” alisema Kent.     

No comments:

Post a Comment

Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina