Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina

Search This Blog

Breaking

Serikali kuja na mpango wa kodi ya nyumba kulipwa mwezi mmoja mmoja

TANGAZA NASI HAPA


2016-02-08

Magufuli: Jibu la mgogoro Z’bar ni kurudia uchaguzi

I

RAIS John Magufuli amesema hatua ya kurudia uchaguzi Zanzibar ndio njia sahihi ya kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani humo. Rais Magufuli aliyasema hayo wakati wa hafla ya kuukaribisha Mwaka Mpya aliyowaandalia mabalozi wanazoziwakilisha nchi zao Ikulu, Dar es Salaam.
Dk Magufuli aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Augustine Mahiga aliyesoma hotuba kwa niaba yake. Alisema kufanyika uchaguzi wa marudio kutasaidia kuondoa mvutano wa kisiasa uliopo na kusisitiza kuwa mazungumzo kati ya vyama vya siasa yaliyoanza Novemba mwaka jana, hayakufikia mwafaka wa namna ya kutatua tatizo hilo.
“Zanzibar ina mfumo wake wa siasa, ina Katiba na ina Tume huru ya Uchaguzi. Hatua ya kufanya uchaguzi ndio njia sahihi katika hali ya sasa katika kumaliza tatizo hilo. “Chama kikuu cha upinzani (CFU) wanadai wameshinda, lakini chama tawala na vyama vingine vinaona haja ya kufanya uchaguzi wa marudio ili kuondoa kasoro,” alisema Dk Magufuli.
Alisema mlango wa mazungumzo juu ya namna ya kufanya uchaguzi wa marudio kuwa huru na haki na kufuata taratibu za kimataifa uko wazi na kuwa ni imani yake nchi marafiki wa Zanzibar na Tanzania wataunga mkono juhudi hizo.
“Kama ilivyo kwa Watanzania wengi wanavyoona, njia ya kuthibitisha ushindi ni boksi la kura na kukataa kushiriki ni kukataa kufikia mwafaka na serikali na kujinyima haki ya miaka mitano ijayo,” alisema Rais.
Aidha, alisema bado kuna siku 40 ambazo zinatosha kuwa na mazungumzo ya kuja na suluhisho la tatizo hilo. Zanzibar inatarajia kufanya uchaguzi wa marudio Machi 20, mwaka huu kutokana na uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana kufutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Mbali ya suala la Zanzibar, Rais Magufuli alizungumzia mambo mengine ikiwamo rushwa, umasikini na ukosefu wa ajira, na kuwaeleza mabalozi hao kwamba nia ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati mwaka 2025 haitafikiwa kama changamoto hizo hazitaondolewa.

1 comment:

Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina