Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina

Search This Blog

Breaking

Serikali kuja na mpango wa kodi ya nyumba kulipwa mwezi mmoja mmoja

TANGAZA NASI HAPA


2016-02-08

Mramba, Yona waanza usafi hospitali


MAWAZIRI wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona wameanza mchakato wa kutumikia jamii kama sehemu ya kifungo chao cha nje baada ya jana kukabidhiwa vifaa vya kufanyia usafi na kuoneshwa maeneo yatakayohusika na usafi huo katika Hospitali ya Sinza, Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa kifungo hicho.
Walibadilishiwa adhabu ya kifungo cha jela na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha nje mwishoni mwa wiki iliyopita na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukamilika mchakato wa kufikia hatua hiyo.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha alisema Sheria ya Huduma kwa Jamii Namba 6 Kifungu Namba 3(1) ya mwaka 2002, inasema mtu yeyote anayetiwa hatiani kwa kosa ambalo adhabu yake ni miaka mitatu kushuka chini, Mahakama inaweza kumpa adhabu ya kutumikia jamii.
Mramba na Yona waliwasili katika eneo la hospitali saa 9:45 asubuhi wakiwa wanatumia gari Toyota Fortuner lenye namba za usajili T222 DCL huku Yona akiwa kiti cha mbele na Mramba akiwa kiti cha nyuma kushoto.
Baada ya kuwasili hapo, tayari kwa kuanza kutumikia adhabu yao ya kifungo cha nje cha huduma kwa jamii, watu walianza kufurika katika eneo hilo wakiwemo wagonjwa hospitalini hapo na wengine kutoka nje ambao walikuwa wakiingia hapo licha ya walinzi kuwazuia bila mafanikio.
Hali hiyo ilipozidi ndipo polisi walipofika wakiwa katika gari lenye namba za usajili PT 3946 na kuwatawanya watu hao na hali kutulia huku mawaziri hao wa zamani wa Fedha na Nishati na Madini, wakienda kuripoti katika ofisi za utawala tayari kwa kuanza kutumikia adhabu yao hiyo.
Yona akiwa mchangamfu kuliko mfungwa mwenzake Mramba walikabidhiwa vifaa mbalimbali vya usafi zikiwemo fyekeo, fagio, majembe, buti, makoti maalumu watakayokuwa wakivaa wakati wa usafi huo, vifaa vya kujikingia vumbi na glovu. Walikabidhiwa na Ofisa Mazingira wa Hospitali ya Palestina-Sinza, Miriam Mongi.
Baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, walitembezwa katika maeneo kadhaa ambayo watatakiwa kufika kila siku na kufanya usafi kwa muda wa saa nne kila siku hadi Novemba 5, mwaka huu ambapo adhabu yao hiyo itakoma. Yona alivaa koti na kushika fyekeo na kujaribu kufyeka huku wanahabari wakipiga picha na Mramba alivunja ukimya uliokuwa umemtawala na kutamka kaulimbiu ya Rais John Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Ofisa Huduma za Jamii wa Hospitali ya Palestina – Sinza, Deogratius Shirima alisema wafungwa hao kabla ya kufika hapo walianzia Mahakama ya Kinondoni ambako walipewa maelekezo ya namna ya kutumikia kifungo chao.
“Kabla ya kuja hapa Yona na Mramba walianzia Mahakama ya Kinondoni ambako walipewa maelekezo ya namna kifungo chao kinavyotakiwa kutekelezwa, walielezwa nini cha kufanya na nini wakifanya watarejeshwa ndani na baadaye wakaja hapa kuoneshwa na kukabidhiwa vifaa vya kazi,” alisema Shirima.
Baada ya kumaliza taratibu zote za makabidhiano ya vifaa na kuoneshwa maeneo ya kutumikia adhabu yao hiyo, wafungwa hao waliondoka hospitalini hapo kwa kutumia gari lao likiongozwa na gari la Polisi saa 5:19 asubuhi.
Leo Mramba na Yona wanataraji kuanza rasmi kutumikia adhabu yao hiyo kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana kila siku, isipokuwa Jumamosi na Jumapili. Aidha, Shirima alisema hukumu hiyo imewavuta watu wengi kwa kuwa tu Yona na Mramba walikuwa ni viongozi na ni watu wenye majina makubwa katika jamii, lakini adhabu kama hiyo inatumikiwa na wananchi wa kawaida zaidi ya 1,000 jijini Dar es Salaam kila siku.
Julai 6, 2015, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwahukumu kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini ya Sh milioni tano, Mramba na Yona huku ikimuachia huru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja baada ya kumuona hakuwa na hatia.
Viongozi hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni iliyopata zabuni ya ukaguzi wa madini ya dhahabu nchini ya M/S Alex Stewart.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa na Hakimu Mkazi Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, Sam Rumanyika ilimtia hatiani Mramba katika mashitaka 11 na Yona mashitaka matano.

No comments:

Post a Comment

Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina