Mtoto wa siku moja ameibwa katika
mazingira ya kutatanisha katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, akiwa pembeni
mwa mama yake aliyekuwa amelala, mwenye umri wa miaka 16.
Akizungumzia uporaji huo jana, Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha, amesema aliyepora mtoto huyo
aliingia ndani ya wodi ya wazazi ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando, akiwa
amejifunga ushungi.
“Alipoingia wodini alikuta mama wa mtoto
amesinzia akiwa peke yake wodini, ndipo akamuiba mtoto wake wa kike mwenye umri
wa siku moja na kuondoka naye kwenda kusikojulikana,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha, Jeshi
la Polisi limeanza uchunguzi wa tukio hilo kwa kuhoji wauguzi, walinzi na
wazazi waliokuwa wamelazwa wodini hapo.
Katika hatua nyingine, Kamanda Kamugisha
amesema Jeshi la Polisi mkoani humo, litaanza kufanya uhakiki wa silaha kuanzia
Aprili mosi hadi Juni 30 mwaka huu, katika ofisi za makamanda wa Polisi wa
wilaya zote za Mkoa wa Mwanza.
Amesema uhakiki wa silaha ni wa kitaifa
na utahusu wamiliki binafsi, kampuni binafsi na taasisi mbalimbali za Serikali
na zisizo za kiserikali zinazomiliki silaha.
“Lengo ni kupata kumbukumbu ya uhalali
wa umiliki wa silaha. Watu wote wanaomiliki silaha watii agizo hili bila
kulazimishwa, ili tufanikishe uhakiki kwa wakati na tuimarishe usalama katika
mkoa wetu,” alisema.
Aliwataka watu wanaomiliki silaha isivyo
halali, kusalimisha silaha hizo wenyewe kwenye ofisi za Serikali na kwa wakuu
wa Polisi wa wilaya (OCD) kabla ya muda wa uhakiki wa silaha kumalizika.
“Baada ya hapo tutafanya msako kabambe wa watu waliokaidi
kuhakiki silaha zao,” alisema.
No comments:
Post a Comment