Msanii wa nyimbo za injili nchini, Rose Mhando,
ameshtakiwa kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye,
kwa kitendo cha utapeli na kushindwa kutekeleza mkataba wa kuhudhuria na
kutumbuiza kwenye Tamasha la Pasaka lililofanyika jijini Mwanza licha ya
kulipwa gharama zote alizotaka.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions
inayoongozwa na Alex Msama, ambayo ina mkataba naye imekuwa ikiuza na kuandaa
matamasha ya msanii huyo pamoja na tamasha la Pasaka la kila mwaka, alimweleza
Waziri Nnauye, mbele ya halaiki ya wananchi alipokuwa mgeni rasmi wa sherehe za
tamasha hilo lililofanyika kwa mara ya kwanza jijini Mwanza na mikoa ya Kanda
ya Ziwa.
Msama alieleza kusikitishwa na kitendo cha Rose
Mhando kuingia mitini ilihali akiwa ameingia mkataba na kulipwa gharama zote
pamoja na nauli alizodai kabla ya kuanza safari kufika Geita, Mwanza na Kahama
kujiunga na wasanii wenzake kwa ajili ya kutumbuiza katika tamasha hilo.
“Mheshimiwa Waziri, Rose Mhando naye amekuwa ni jipu
kwa kuwa amefanya utapeli kwa kukubali kulipwa gharama zake zote lakini
ameshindwa kuhudhuria na kutumbuiza kama wenzake wakina Solomon Mkubwa, Bonny
Mwaitege, Upendo Nkone na wengine uliowashuhudia hapa.
“Hii ni mara ya tatu amekuwa akifanya hivi na mara
kwa mara nimekuwa nikimsamehe,” alisema bila kutaja kiasi alichomlipa katika
mkataba waliokubaliana ili aweze kufanya onyesho hilo.
Msama pia akatumia fursa hiyo kuwaomba radhi
wananchi waliofika katika Uwanja wa CCM Kirumba kwa kutegemea mwimbaji huyo
angekuwepo na kutumbuiza na wenzake lakini kilichotokea ni aibu na utapeli wa
msanii huyo mkubwa wa nyimbo za injili aliyejizolea umaarufu ndani na nje ya
nchi.
“Kuanzia leo mtu yeyote asije akaingizwa mjini na
Rose Mhando kwa kuingia naye makubaliano akidhani yupo chini ya Kampuni ya
Msama Promotions, kwa kitendo alichoendelea kukifanya naomba kutangaza rasmi
kuvunja mkataba wa kufanya kazi na msanii huyo ili kulinda hadhi na heshima ya
Kampuni yangu,” alisisitiza Msama.
Msama aliomba wananchi waendelee kuipa sapoti
kampuni yake kwa kuwa imekuwa ikirejesha mapato ya viingilio na sadaka katika
tamasha hilo kwa jamii hasa kwa watu wasiojiweza, makundi maalumu pamoja na
kuendeleza vipaji vya wasanii chipukizi wa nyimbo za injili nchini kote.
Hata hivyo, wadau mbalimbali waliokuwepo katika
uzinduzi huo walisikitishwa na kutokutokea kwa mwanamuziki huyo huku wengine
wakimlalamikia kuwa na tabia hizo kwa muda mrefu na kufanya bila woga na hofu
yoyote.
Mwanamuziki huyo aliwahi kuripotiwa kutuhumiwa
kufanya udanganyifu kwa kupokea zaidi ya Sh milioni 3 na kisha kushindwa
kufanya onyesho katika tamasha la nyimbo za injili lililoandaliwa mkoani Njombe
mwaka jana.
Mkurugenzi wa Kampuni ya The Comfort Gospel Promotions,
Seth Sedekia, ndiye alimfungulia kesi hiyo katika kituo kikuu cha polisi
Njombe na akapewa RB namba: NJ/RB/1793/2015.
Kushindwa kutokea kwa mwanamuziki huyo siku hiyo ya
Jumapili iliyopita, kuliwafanya mashabiki waliokuwa wamelipa kiingilio cha
shilingi 5,000 kila mmoja kuzusha vurugu kubwa kwa mwandaaji huyo wakidai
wametapeliwa huku wengine wakionyesha kuchukizwa na kitendo cha mwanamuziki
huyo kushindwa kutokea kufanya onyesho hilo.
Mwandaaji wa onyesho hilo, Sedekia alisema amefikia
hatua ya kufungua kesi kituo cha polisi kufuatia kumlipa fedha zote shilingi
milioni tatu Mhando ambazo alisaini mkataba naye akiwa mjini Dodoma kwa
ajili ya kufanya onyesho mjini Njombe. Katika onyesho hilo, Mhando alitarajiwa
kushirikiana na msanii wa nyimbo za injili, Happy Kamili kutoka jijini Mbeya
ambaye alifika katika tamasha hilo akishirikiana na wasanii wengine kutoka
mjini Njombe.
Ofisa Habari wa Kamanda wa Polisi mkoani Njombe,
Franco Malimba, alipoulizwa juu ya kuwepo kwa taarifa hizo katika kituo cha polisi,
alikiri kuwepo lakini alisema hawezi kulizungumzia kwa sababu halijafika ngazi
za juu.
No comments:
Post a Comment