Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina

Search This Blog

Breaking

Serikali kuja na mpango wa kodi ya nyumba kulipwa mwezi mmoja mmoja

TANGAZA NASI HAPA


2016-07-16

RAIS MAGUFULI ATOA SH BIL 12.3 KUKARABATI MAHAKAMA


JAJI Mkuu, Mohamed Chande Othman amempongeza Rais John Magufuli kwa kutoa zaidi ya Sh bilioni 12.3 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya mahakama nchini.

Ametoa pongezi jana wakati akizindua Mahakama ya Wilaya ya Siha na Mahakama ya Mwanzo Bomang’ombe, iliyopo wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Jaji Chande, ujenzi huo utaanza hivi karibuni kwa wilaya na mikoa ambayo hazina huduma hiyo, ili kusogeza huduma za mahakama karibu na wananchi, hali itakayosaidia kupunguza mrundikano wa kesi katika mahakama nyingine.

Wilaya 26 na mikoa sita hapa nchini, zinakabiliwa na ukosefu wa huduma za mahakama za wilaya pamoja na mahakama kuu, hali inayosababisha wananchi kutumia gharama kubwa kutafuta huduma hiyo katika wilaya na mikoa mingine.

Alieleza kuwa fedha zilizotolewa na Rais Magufuli, zitakwenda kwenye ukarabati na ujenzi wa mahakama za mwanzo, ili watendaji wa mahakama hizo wafanye kazi katika mazingira bora, ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa mahakimu na makarani wa kutosha.

Alisema mbali na fedha hizo, pia anaishukuru serikali kwa kuongeza bajeti ya idara ya mahakama kwa mwaka wa fedha 2016/2017, ambapo wanakusudia kujenga mahakama za wilaya 10, Mwanzo 10, ambapo alitaja baadhi ya mikoa ambayo haina Mahakama Kuu kuwa ni mkoa wa Singida, Lindi na Mara.

Alisema asilimia 74 ya kesi za mashauri yapo katika mahakama za mwanzo, ambapo mashauri zaidi ya 1,150 yanayosikilizwa katika mahakama hizo hapa nchini, ambapo aliziagiza mahakama za mwanzo na wilaya kuhakikisha kesi zote za mashauri zinafunguliwa katika mahakama hizo.

Aliagiza ifikapo mwisho wa mwaka huu, hataki kuona wala kusikia kesi iliyomaliza muda wa miezi sita bado inaendelea kupoteza muda na gharama bila ya sababu za msingi, na kutoa wito kwa jeshi la polisi kujitaidi kukamilisha upelelezi wa kesi ili kuwajengea wananchi imani na kutoa fursa kwao kudai na kupata haki zao mahakamani kwa wakati.

Awali Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi, Jaji Aishieli Sumari, alisema changamoto inayoikabili idara ya mahakama ni pamoja na ukosefu wa watumishi na mahakimu katika wilaya ya Siha, ambapo mahakama hiyo tangu kufunguliwa kwake Aprili 4 mwaka huu, tayari imepokea mashauri 87 na yaliyosikilizwa ni 19 kutokana na wilaya kutokuwa na hakimu.

Jaji Sumari alisema Mahakama ya Mwanzo Bomang’ombe imepokea mashauri 285 kuanzia Juni mwaka 2015 ambapo makosa ya jinai yalikuwa 239, talaka sita, mirathi 33, na kesi za madai 15, ambapo hadi sasa mashauri 10 yalikuwa bado hayajamalizika ndani ya miezi sita, tangu kufunguliwa kwa mashauri hayo.

No comments:

Post a Comment

Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina