MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli amesisitiza kutekelezwa kwa mpango wa serikali kuhamishia makazo yake mkoani Dodoma ndani ya kipindi cha miaka mitano ya utawala wake huku akitangaza kuigeuza Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam kuwa sehemu ya maonyesho.
Aidha, Rais Magufuli amesema majengo ya wizara mbalimbali yaliyopo karibu na mwambao wa Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam yatauzwa kwa wawekezaji mbalimbali ili yageuzwe hoteli za kitalii na fedha zitakazopatikana zitatumika kuustawisha mji wa Dodoma ambako serikali inahamia.
Magufuli alitangaza mpango huo jana wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa chama hicho muda mfupi baada ya kutembelea ofisi yake ya kichama iliyopo ndani ya jengo la Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli alisema wale wanaosema kuwa amesema atauza Ikulu baada ya kuhamia Dodoma wanapotosha ukweli kwa sababu serikali haina mpango huo.
“Wengine wanasema Ikulu itauzwa.. jengo la Ikulu litabaki pale, litakuwa jengo la maonyesho… wizara na majengo mengine yaliyo jirani na bahari yatauzwa ili tupate fedha za kuiendeleza Dodoma,” alisema Magufuli.
Alisema Serikali inahamia Dodoma ili Dar es Salaam ipumue na ili viongozi wakitaka kuja waje kwa ajili ya kutembea lakini shughuli zote za Serikali zitakuwa zimehamia mkoani humo.
Aidha, Rais Magufuli aliwashangaa watu wanaokejeli mpango wake wa kuhamishia Serikali Dodoma na kubeza kwa kudai kuwa haiwezekani.
“Suala la kuhamia Dodoma limeanza tangu mwaka 1973. Nimesoma darasa la kwanza hadi Chuo Kikuu, nikamaliza bado hatujahamia… hatuwezi kujenga Serikali kwa mchakato, mchakato umekwisha, nimesema ndani ya miaka minne na miezi minne iliyobaki, nitahikikisha tutakuwa tumeshaondoka Dar es Salaam,” alisisitiza.
Alishangaa pia watu wanaohoji kwamba watapata wapi makazi iwapo Serikali itahamia mkoani humo na kuhoji kuwa mbona wakati wa Bunge watumishi hao hao huwa wanakwenda kwa wingi na wanapata makazi.
“Wakati wa Bunge, zaidi ya watu 300 huwa Dodoma, mawaziri, manaibu na makatibu wakuu, wanakaa na wanatosha… kwa nini hili wanahoji watakaa wapi,” alisema.
“Nazifahamu ofisi zote ukitoka Hoteli ya Kilimanjaro mbele kuna ofisi ya Takwimu, Wizara Ardhi, Utumishi zote zimetazama baharini… tutatangaza zabuni watu wanaotaka kujenga hoteli watanunua huko kote kuwe eneo la kitalii, tukipata fedha tutaweka makandarasi kujenga Dodoma. Hakuna kinachoshindikana, kinashindikana kwenye akili zetu,”alisema.
Aidha, alisema awali wakati wakitangaza kwenda Dodoma, kulikuwa hakuna miundombinu, maji, umeme wala barabara lakini sasa kila kitu kipo na mipango ya kuiboresha Dodoma ipo.
Alisema Dodoma ikijengwa miji mingine itakuwa na utalii utaongezeka kwa sababu huo (Dodoma) ni mji ambao upo katikati ya nchi.
“Kutoka Dodoma kwenda Arusha ni saa moja na nusu na maeneo mengine hii itasaidia watu wa mikoa mbalimbali kuja kuwekeza Dodoma na wamachinga nao watakuja,” alisema.
No comments:
Post a Comment