WAZIRI wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesitisha ajira ya Mkurugenzi
Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), George Nyatega
kwa tuhuma za udhaifu katika fedha za mikopo zaidi ya Sh bilioni 3.2.
Pia
amewasimamisha kazi wakurugenzi watatu wa Fedha na Utawala, Urejeshaji Mikopo
na Upangaji na Utoaji Mikopo katika HESLB kwa tuhuma za udhaifu huo wa mikopo
ya Sh 3,234,452,259.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Profesa Ndalichako alisema hatua
hiyo, imechukuliwa baada ya kuridhika na kuona utendaji usioridhisha kwenye
taasisi hiyo, kiasi cha kuwapo matatizo mengi yanayojirudiarudia kwa wateja
wao, ikiwamo ucheleweshaji wa mikopo bila sababu ya msingi.
Profesa
Ndalichako alisema pia uongozi wa bodi hiyo, umeshindwa kutoa majibu ya Mkaguzi
wa Ndani Mkuu wa Serikali, alipoagizwa na Wizara Januari mwaka huu.
“Majibu
yaliyowasilishwa na Bodi Februari 1, mwaka huu yanadai kuwa taarifa ya mkaguzi
haikukidhi viwango na kwamba ilijikita katika ‘operational audit’, wakati kazi
hiyo hufanywa na mkaguzi wao wa ndani. Pia walikiri baadhi ya udhaifu kama
kusajili mara mbili ambao ulitokana na kuwa wakati huo walikuwa hawajaanza
kutumia mfumo wa kompyuta,” alieleza Waziri wa Elimu.
Aliongeza:
“Kwa mamlaka niliyopewa kwa mujibu wa Kifungu D.5(3) cha Kanuni za Kudumu
kinachohusu uteuzi wa maofisa wa juu wa taasisi za serikali na Kifungu D.12
kinachoruhusu utoaji wa taarifa za Mtendaji na Kifungu F.50(1) kinachohusu
usitishaji wa mkataba na kile cha Bodi ya Mikopo Kifungu cha 11(3), nimesitisha
mkataba wa ajira wa George Nyatega,” alieleza Profesa Ndalichako.
Alisema
kutokana na kusitisha ajira ya kiongozi huyo, Bodi inatakiwa kumlipa mshahara
wa mwezi mmoja kama notisi kulingana na Kifungu 50(3)(a) cha Kanuni za Kudumu.
Nyatega alikuwa astaafu Agosti 31, mwaka huu baada ya kuwa aliongezewa mkataba
wa miaka miwili baada ya kustaafu Machi 2014, na kuongezewa mkataba kuanzia
Septemba 2014.
Alisema
pia amewasimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusufu Kisare,
Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo Juma Chagonja na Mkurugenzi wa Upangaji na
Utoaji Mikopo, Onesmo Laizer na kuwa wizara itateua maofisa watakaoshika nafasi
hizo hadi uchunguzi utakapokamilika na wakurugenzi hao kuchukuliwa hatua
stahiki.
“Namwagiza
Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali ahakiki maelezo na nyaraka zilizowasilishwa
na Bodi ya Mikopo pamoja na kufanya ukaguzi maalumu kwa kipindi cha kuanzia
mwaka 2013 hadi sasa ukaguzi uanze mara moja,” alieleza Profesa Ndalichako.
Akifafanua
zaidi kuhusu malipo yasiyo sahihi, alisema: “baadhi ya wanafunzi ambao
walikwenda kusoma Algeria wamekuwa wakiendelea kulipwa fedha wakati mkataba wao
wa mkopo wa miaka minne umekwisha, lakini wamelipwa hadi miaka saba kinyume cha
utaratibu.”
Alisema
ukaguzi huo wa mwaka 2013, umebainisha kuwa wanafunzi 23 walipata mikopo
kupitia vyuo viwili tofauti na walilipwa jumla ya Sh 153,999,590 katika chuo
kimoja na Sh 147,541,460 katika chuo cha pili ambazo zimelipwa miaka mitatu
mfululizo.
Waziri
alisema pia wanafunzi 169 walilipwa mikopo kupitia vyuo viwili tofauti ambapo
Sh 658,047,570 zililipwa katika chuo cha kwanza na Sh 665,135,716 chuo cha pili
zilizolipwa kwa miaka miwili mfululizo.
Alisema
pia wanafunzi 343 wasiokuwa na usajili kwenye vyuo husika walilipwa Sh 342,468,500
huku wanafunzi 55 walioacha masomo walilipwa Sh 136,232,800.
“Jumla
ya Sh 159,664,500 zililipwa kwa wanafunzi 306 zaidi ya kiwango kilichobainishwa
kwenye vipengele namba 4.3 na 4.3.2 cha miongozo ya upangaji na ukopaji ya
mwaka 2008/2009 na 2009/2010 na vipengele no 4.6 na 4.3.1 cha miongozo ya
upangaji na ukopeshaji mikopo ya mwaka 2008.2009 na 2009/2010 hadi
2010/2011."
Alifafanua
kuwa pia wanafunzi 77 walipatiwa mikopo kwenye vyuo vya ndani na nje ya nchi
kwa wakati mmoja.
Wanafunzi
hao walitumiwa Sh 467,620,654 kwa vyuo vya nje na Sh 123,047,119 ya vyuo vya
ndani huku wanafunzi 19,348 walipatiwa mikopo bila kupitishwa na Kamati ya
Mikopo wakati wanafunzi 54,299 walipangiwa mikopo wakati hawakuwa wameomba.
Alisema
kuwa pia Bodi ilipeleka Sh 207,052,650 kwenye vituo sita vya elimu ya juu na
kutochukuliwa na wanafunzi husika na fedha hizo hazikurejeshwa Bodi kinyume cha
Hati ya Makubaliano (MOU) kifungu 3.3.4(b) na (c).
“Ukaguzi
utakwenda mpaka kwenye vyuo, endapo tutabaini vyuo kiwe cha umma au binafsi
wamehusika kushirikiana na watendaji wa Bodi kuhujumu fedha tutachukua hatua za
kisheria dhidi yao. “Nazionya taasisi zilizo chini ya wizara, sitakuwa tayari
kuona wanafunzi wanakaa chini, hawana madarasa halafu kuna taasisi zinahujumu
hata senti tano, tutaendelea kuzifuatilia kwa karibu,” alionya Profesa
Ndalichako.
Katika
hatua nyingine, Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limekanusha taarifa
zilizosambazwa jana katika mitandao ya kijamii kuwa limezuia matokeo hadi
yasahihishwe upya, kuwa si za kweli na kwamba mchakato wa kutunuku uko katika
hatua nzuri; kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi.
No comments:
Post a Comment