Dk Asha-Rose Migiro
Rais Dk John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa mabalozi watatu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa. Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, imewataja mabalozi walioteuliwa kuwa ni Dk Asha-Rose Migiro, Mathias Chikawe na Dk Ramadhan Dau.
Vituo vya uwakilishi kwa mabalozi hao vitajulikana baada ya taratibu husika za kidiplomasia kukamilika.
Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano – Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa makamishna wanne wa Jeshi la Polisi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Kwa upande wa Makamishna wa Polisi, Balozi Sefue amewataja walioteuliwa kuwa ni Naibu Kamishna wa Polisi Simon Nyakoro Sirro ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi, na ameteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam. Kamishna Sirro anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Mstaafu Suleiman Kova. Makamishina wengine walioteuliwa na nyadhifa zao kwenye mabano ni Naibu Kamishna wa Polisi Albert Nyamuhanga (ataongoza Idara ya Fedha, Utawala na Lojistiki), Kamishna Nyamuhanga anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna wa Polisi Clodwing Mathew Mtweve aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza.
Wengine ni Naibu Kamishna wa Polisi Robert Boaz Mikomangwa ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi (ataongoza Idara ya Intelijensia), Kamishna Mikomangwa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Valentino Mlowola aliyeteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Nsato Marijani Mssanzya ambaye amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza Idara ya Mafunzo na Operesheni.
Aidha, Rais Magufuli amemteua Dk Modestus Francis Kipilimba kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Kabla ya Uteuzi huu Dk Kipilimba alikuwa Mkurugenzi wa Menejimenti ya Udhibiti katika Benki Kuu ya Tanzania, Dk Kipilimba anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Dikson Maimu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa