Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande
wa mashtaka kukamilisha upelelezi haraka ili kesi inayowakabili wabunge watatu
wanaotokana na Ukawa na madiwani wao ianze kusikilizwa.
Washtakiwa hao ni pamoja na Mbunge wa Kawe,
Halima Mdee, Mwita Waitara (Ukonga) na Saed Kubenea (Ubungo).
Madiwani wanaoshtakiwa katika kesi hiyo ni
Ephrein Kinyafu (Kimara), Manase Njema (Kimanga, Tabata) na kada wa chama
hicho, Rafii Juma.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alitoa kauli hiyo
jana baada ya Wakili wa Serikali, Mbunito Aloyce kudai kesi ilikuja kwa ajili
ya kutajwa kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika na kuomba ipangiwe tarehe
nyingine.
Wakili Peter Kibatala anayewatetea washtakiwa
hao, aliuomba upande wa mashtaka kuanza kuisikiliza kesi hiyo kwa sababu
washtakiwa walikamatwa haraka haraka na usikilizaji wake uwe vivyo hivyo.
Washtakiwa hao wanaodaiwa kumjeruhi Katibu Tawala
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresa Mmbando katika vurugu zilizotokea Februari
27,2016 Ukumbi wa Karimjee kwenye Uchaguzi wa meya na naibu meya wa jiji la Dar
es Salaam, wanatetewa na Mawakili Peter Kibatala na John Malya. Kesi hiyo
imeahirishwa hadi Aprili 18. \\\\
No comments:
Post a Comment