Watu wawili wamefariki
dunia na wengine 13 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Ndenjela linalofanya
safari zake kati ya Mbeya na Dar es Salaam kuligonga kwa nyuma basi dogo aina
ya toyota Hiace ambalo ni daladala linalofanya safari zake kati ya Igawilo na
stendi kuu jijini Mbeya katika eneo la Uyole, kwenye barabara kuu ya Tanzania -
Zambia.
Ajali hiyo imetokea majira ya alfajiri wakati
basi la kampuni ya Ndejela likitokea gereji kwenda katika kituo kikuu cha
mabasi jijini Mbeya kwa ajili ya kuchukua abiria ili kuanza safari ya kwenda
Dar es Salaam, lakini lilipofika eneo la Kilimo katika bonde la Uyole, ndipo
basi dogo aina ya toyota Hiace ambalo lilikuwa limesimama kituoni,likaingia
ghafla barabarani na ndipo lilipogongwa na kwa nyuma na basi hilo la Ndenjela
ambalo lilikuwa kwenye mwendo mkali na kusababisha daladala hilo kuacha njia na
kugonga jiwe kubwa kando ya barabara.
Afisa muuguzi msaidizi wa zamu katika
hospitali ya rufaa Mbeya,Abdul Kumwambe amethibitisha kuwepo kwa vifo vya watu
wawili pamoja na majeruhi 13 ambao wanatokana na ajali hiyo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya,Kamishna
msaidizi mwandamizi wa jeshi la polisi,Ahamed Msangi amesema kuwa chanzo cha
ajali hiyo ni mwendo wa kasi wa basi la kampuni ya Ndenjela huku akidai kuwa
uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea.
No comments:
Post a Comment