Matukio ya wajawazito kupoteza watoto kwa madai ya uzembe wa
wahudumu wa afya yameendelea kuugubika Mkoa wa Mwanza baada ya mkazi wa
Nyarawambo wilayani Sengerema Tatu Muhangwa, kujifungua na mtoto wake kufariki
kwa kukosa huduma.
Mama mzazi wa Tatu, Vumilia Nailon alisema mjukuu wake alifariki
baada ya wahudumu wa afya katika Zahanati ya Ngoma ‘B’ iliyopo Kata ya
Nyamatongo wilayani Sengerema, kuchelewa kumhudumia.
Mhudumu wa afya aliyekuwa zamu, Helena Mulwisha alisema
alishindwa kumhudumia mjamzito huyo kutokana na kubaini kuwa mtoto alikuwa
kakaa vibaya tumboni na kuwashauri kumpeleka hospitali ya wilaya kwa msaada
zaidi.
Nailon alisema: “Nilimfikisha mgonjwa wangu zahanati
juzi, saa kumi na moja alfajiri, lakini hadi saa tatu hakuwa amepatiwa huduma
yoyote hadi alipojifungua mwenyewe bila msaada na mtoto kufariki.
“Mmoja wa wahudumu wa afya aliyekuwapo alishindwa kumhudumia
baada ya kugundua mtoto amekaa vibaya tumboni na yeye hana utaalamu wa
kumsaidia.”
Alisema Mulwisha aliwashauri kumpeleka mgonjwa hospitali ya
wilaya kwa sababu wauguzi na madaktari walikuwa wakihudhuria semina.
“Baada ya kukosa gari ya kumuwaisha hospitali, tuliamua kutembea
kwa miguu umbali wa kilomita mbili, lakini hatukufika baada ya magonjwa wangu
kujifungulia njia kwa msaada wa wasamaria wema na mtoto kufariki,” alisema Vumilia.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Dk Henry Nyamete
alisema ofisi yake inachunguza tukio hilo na kwamba itachukua hatua za
kinidhamu dhidi ya mhudumu wa afya aliyekuwa zamu siku hiyo kwa kushindwa
kuwajibika kwa kuita gari la wagonjwa ili kumuwahisha mjamzito huyo hospitali
kwa matibabu zaidi.
No comments:
Post a Comment