Wakati sakata la Kampuni ya Lugumi kudaiwa kushindwa kutekeleza mradi wa
utambuzi wa vidole kwenye vituo vya polisi likianza kudaliwa na Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles
Kitwanga amesema hana uhusiano wowote na kampuni hiyo kama watu wanavyodai.
Kitwanga ambaye alihusishwa na Lugumi kupitia kampuni ya Infosys
iliyodaiwa kwamba kiongozi huyo ni mmoja wa wanahisa wakati akiwa mfanyakazi wa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ameeleza kuwa hahusiki na wala halijui suala la
Lugumi.
Infosys ambayo imekanusha kuhusika katika sakata hilo imedaiwa
kuwa iliisaidia kampuni ya Lugumi kupata vifaa kutoka kampuni ya Dell ya
Marekani ili viweze kufungwa kwenye vituo vya polisi.
Jana Kitwanga alisema anashangazwa jinsi anavyohusishwa kwa
maelezo kuwa wakati tukio hilo likitokea mwaka 2011, yeye hakuwa waziri wa
wizara hiyo.
“Inanishangaza sana
sihusiki na wala silijui hili suala la Lugumi. Wakati linatokea sikuwa waziri
wa wizara hii ndiyo maana huwa sipendi na wala sitaki kuzungumza chochote
kuhusu Lugumi,” alisema.
Kitwanga alifafanua kuwa baadhi ya mambo yameanza kubainika
baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, licha ya kutotaka
kuweka wazi kama suala la Lugumi ni miongoni mwa mambo hayo.
Kampuni ya Lugumi ilibainika kutotimiza matakwa ya mkataba wake
baada ya kufunga mashine 14 tu kati ya 108 zilizotakiwa kufungwa, licha
ya kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya fedha kwa mujibu wa mkataba.
Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka
2013/14 ndiyo iliyofichua udhaifu huo.
Utekelezwaji wa mkataba huyo uliwasilishwa jana kwa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na mwenyekiti wake Aeshi Hilaly alisema
wameanza kuupitia na watakapokamilisha wataweka kila kitu wazi.
Kwa upande wake Ndugai alipotakiwa kuzungumzia suala hilo
alisema, “Mimi sijapata taarifa zozote za Lugumi. Jambo hilo bado lipo
katika kamati ya bunge.”
No comments:
Post a Comment