Maziko ya mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi
wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba yatafanyika kesho mkoani
Morogoro baada ya kukamilika kwa taratibu za kuaga mwili wake leo jijini Dar es
Salaam.
Liyumba alifariki dunia juzi saa 10.00 jioni katika Hospitali ya
Aga Khan kutokana na maradhi ya kisukari na shinikizo la damu ambayo yamekuwa
yakimsumbua kwa muda mrefu mpaka dakika ya mwisho.
Akizungumzia taratibu za mazishi, msemaji wa familia, Moses
Liyumba alisema marehemu atazikwa nyumbani kwake Morogoro.
“Marehemu alilazwa
katika Hospitali ya Aga Khan siku tatu kabla ya kufariki dunia. Bado tunaandaa
utaratibu wa kuaga mwili kisha kuelekea Morogoro kwa ajili ya maziko,” alisema Moses nyumbani kwao Kawe
Avocado.
Moses, ambaye ni mtoto mkubwa wa Liyumba, alisema marehemu baba
yake ameacha watoto saba aliozaa na mke wake aliyefariki dunia mwaka
2005.
“Tunasikitika kwa kifo
cha mzee wetu, lakini ndiyo mapenzi ya Mungu. Watoto wake wote tupo, na wengine
wawili wanaoishi nje ya nchi wameshafika kwa ajili ya kumpumzi- sha mpendwa
baba yetu.”
Mkurugenzi huyo wa zamani wa BoT aliandikwa sana kwenye vyombo
vya habari mwaka 2009 alipokuwa anakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi
kati ya mwaka 2001 na 2006 wakati wa ujenzi wa majengo pacha ya makao makuu ya
BoT.
Siku ya hukumu ya kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, shtaka la kuisababishia Serikali hasara ya Sh221 bilioni lilitupwa,
lakini alitiwa hatiani kwa shtaka la matumizi mabaya ya madaraka. Liyumba
alitiwa hatiani Mei 23, 2010 kwa kosa hilo na kufungwa miaka miwili jela mpaka
Septemba 24, 2011 alipoachiwa huru.
No comments:
Post a Comment