Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina

Search This Blog

Breaking

Serikali kuja na mpango wa kodi ya nyumba kulipwa mwezi mmoja mmoja

TANGAZA NASI HAPA


2016-06-17

MJADALA WA MIKOA MASIKINI WALIGAWA BUNGE

TAKWIMU kuhusu mikoa mitano masikini zaidi nchini, zimezidi kuzua mjadala bungeni huku wabunge wakizitumia kutaka misaada zaidi katika mikoa yao na wengine wakidai zinawafanya wahofu kwamba kuna ajenda ya siri kwani hawaamini usahihi wake.


Katika mjadala wa jana kuhusu bajeti inayopendekezwa na serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, aliyeanza kulalamikia takwimu hizo na kukataa kuunga hoja hiyo ya serikali ni Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengelwa.

Mbunge huyo wa CCM alisema katika utafiti wake, amegundua kwamba waziri alipata takwimu hizo kutoka halmashauri, lakini akasema yeye ametafiti na kugundua kwamba kamwe Pwani haiwezi kuuzidi mkoa wa Mwanza kwa utajiri kama takwimu hizo zinavyoonesha.

Alisema takwimu hizo zinaonesha kana kwamba mkoa wa Pwani, una hali nzuri wakati si kweli, kwani hali ni mbaya, vyama vya msingi takribani vyote vimeanguka na kwamba anapata hisia kuwa takwimu hizo, zimetumiwa kuinyima Pwani mambo mengi katika bajeti inayopendekezwa.

“Rufiji, kwa mfano haijawahi hata kupelekewa trekta… Hali ni mbaya na hata bajeti kwa ajili ya kuinua kilimo Rufiji hakuna. Mimi kama mwanasheria niko tayari kuapa kuonesha kwamba takwimu alizotumia Waziri si sahihi,” aling’aka.

Naye Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM), alisema anadhani mkoa wa Pwani umewekwa kwenye kundi la mikoa tajiri kwa bahati mbaya, kwani akitazama kila kitu hakiendi vizuri.

“Hata korosho ambalo ndilo zao kuu la biashara mkoa wa Pwani tuko chini, hatuwezi kulingana na wenzetu wa Lindi au Mtwara,” alisema na kutaka waziri aeleze vigezo vilivyotumika kuainisha mikoa yenye hali mbaya kiuchumi nchini na yenye hali nzuri.

Lakini Mbunge wa Nyamagana mkoa wa Mwanza, Stanslaus Mabula (CCM), alitumia takwimu hizo kutaka serikali kuanza kwa kuupa mkoa huo Sh milioni 50 zilizoahidiwa katika kila kijiji ili wananchi wa mkoa huo wapunguze ‘umasikini wao’.


 “Ninaomba hizi shilingi milioni 50, zianzie katika mikoa iliyoainishwa kuwa masikini kwa mujibu wa takwimu za waziri ukiwemo mkoa wangu wa Mwanza,” alisema Mabula.

Naye Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jason Rweikiza alitumia takwimu hizo kutaka serikali kuwaondolea wakulima wa kahawa kodi 26 wanazolazimika kulipa pamoja na kudhibiti ugonjwa wa mnyauko unaoshambulia migomba ili kuwaokoa wananchi wa Kagera na umasikini.

“Kahawa inakatwa kodi 26, kwa nini wananchi wasiwe masikini? Migomba inaelekea kumalizika kabisa kwa sababu ya ugonjwa wa mnyauko, kwa nini wananchi wasiwe masikini,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Maria Kangoye anayewakilisha mkoa wa Mwanza alipinga takwimu zinazoonesha kwamba mkoa huo ni miongoni mwa mikoa mitano masikini nchini.

Alisema takwimu za Benki Kuu (BoT) zinaonesha kwamba Mwanza ni mkoa wa pili nyuma ya Dar es Salaam katika kuchangia kwenye Pato la Taifa.

Akiwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi ya Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/17, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitaja mikoa masikini zaidi kuwa ni Kigoma, Geita, Kagera, Singida na Mwanza; wakati mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Pwani na Manyara ndiyo mikoa mitano yenye ahueni ya umasikini nchini.

Akiuliza swali la papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Oscar Mukasa (CCM), alisema utafiti kuhusu kipato cha kaya, umebaini mikoa mitano inayokabiliwa na umasikini uliokithiri na kumtaka Majaliwa kueleza serikali itafanya nini katika mikoa hiyo ili iondokane na aibu wakati ina fursa za kiuchumi ikiwemo kilimo cha pamba, mibuni na michikichi.

Majaliwa alisema serikali haijaacha jambo hilo kama lilivyo, bali imekuwa ikishawishi wananchi kujianzishia miradi na wengine waunde vikundi, ikiwemo vya Vicoba ili kujijengea mtaji wa pamoja ili waanzishe miradi hiyo.

Alisema kwa Tanzania msingi mkubwa wa kuondokana na umasikini ni kilimo na maeneo ya kulima yapo, ndio maana Serikali inasema ‘Hapa Kazi Tu’ ili watu wajikite katika kilimo.

No comments:

Post a Comment

Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina