Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema Demokrasia, Katiba na Sheria haziheshimiwi na kwamba Jeshi la Polisi limekuwa wakala wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kilichofanywa kwenye uchaguzi wa umeya wa Manispaa ya Kinondoni kinawapa sababu ya kurejea operesheni yao wanayoiita Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (UKUTA).
Mbowe
amesema hayo Oktoba 23, 2016 alipofika eneo ulipofanyika uchaguzo wa
Meya Kinondoni ambapo madiwani wa Ukawa walisusia uchaguzi huo na kudai
kwamba Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Aron Kagurumjuli, ameshirikiana
na CCM kuhujumu zoezi hilo, hivyo wametangaza kwenda mahakamani kupinga
uchaguzi huo baada ya CCM kuendelea na uchaguzi huo na kutangaza
mshindi.
Njama
zinazodaiwa kufanywa na mkurugenzi huyo ni kugawanya madiwani kinyume
na kanuni kwa kuhamisha madiwani wa upinzani kwenda Halmashauri ya
Ubungo na kuwahamishia Kinondoni madiwani wa CCM kutoka halmashauri
nyingine.
Mbowe
amesema Serikali inaendeshwa kwa hila kwani licha ya uchaguzi kufanyika
siku ambayo si ya kazi, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, alikataa barua
iliyoandikwa na madiwani Jumamosi Oktoba 22 kuzuia uchaguzi huo kwa
kudai kuwa si siku ya kazi.
Aliendelea
kwa kumlaumu Rais Dk. John Magufuli kwamba ameanzisha utamaduni wa
kuuwa demokrasia na kwamba analiletea taifa madhara makubwa.
Kwa
upande wake Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), amesema wametoka
kwenye uchaguzi huo baada ya baadhi ya madiwani wao kuzuiwa kuingia
kwenye kikao hicho.
Mdee alisema kuwa CCM wameingiza madiwani ambao si wajumbe halali wa kikao hicho kwasabau wanatoka katika halmashauri zingine.
“Humo
ndani yumo Profesa Joyce Ndalichako ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na
alisajiliwa kama mkazi wa Ilala na alipiga kura za umeya Ilala hivyo
mnaweza kuona uhuni unaofanywa.
“Lakini
yumo pia Tulia Akson (Dk. Tulia Akson, Mbunge wa Kuteuliwa na Naibu
Spika) ambaye si mkazi wa Kinondoni yeye amesajiliwa kama mkazi wa
Ubungo,” alisema Mdee.
Amesema
kwa mujibu wa kanuni Halmashauri moja haiwezi kuwa na wabunge wa
kuteuliwa zaidi ya watatu na kueleza kuwa katika kikao hicho wamo
wabunge wanne wa kuteuliwa.
Hivyo, kutokana na hali hiyo Mdee amesema watakwenda mahakama ili kupata tafsiri za kisheria za suala hilo kupata haki.
No comments:
Post a Comment