Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina

Search This Blog

Breaking

Serikali kuja na mpango wa kodi ya nyumba kulipwa mwezi mmoja mmoja

TANGAZA NASI HAPA


2016-09-02

Rais Magufuli Awasili Pemba Kwa Ziara Ya Kikazi Ya Siku Mbili

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Asubuhi ya leo tarehe 02 Septemba, 2016 amewasili Kisiwani Pemba ambapo majira ya Alasiri anatarajiwa kuzungumza na wananchi wa Pemba katika Mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa Gombani ya Kale kisiwani hapa.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Pemba kwa Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ameelekea katika kijiji cha Wawi Bigilini kilichopo katika Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba ambako amezulu Kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marehemu Dkt. Omar Ali Juma.

Dkt. Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli wameweka mashada ya maua katika Kaburi la Marehemu Dkt. Omar Ali Juma na wameshiriki Dua ya kumuombea Marehemu iliyoongozwa na Viongozi wa Madhehebu ya Dini ya Kiislamu na Kikristo.

Akizungumza mara baada Dua, Rais Magufuli amesema anamkumbuka Marehemu Dkt. Omar Ali Juma kwa ukarimu wake, upendo, kutojikweza, kutobagua watu na kudumisha amani katika siku zote za maisha yake.

Dkt. Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kudumisha kwa vitendo amani aliyoisimamia Marehemu Dkt. Omar Ali Juma.

"Mimi najua huko aliko Marehemu Dkt. Omar Ali Juma anaendelea kuliombea Taifa hili ili hiyo amani aliyoihubiri katika maisha yake, ili huo upendo aliousimamia katika maisha yake, ili huo uchapa kazi kwa ajili ya manufaa ya watanzania wote tuweze kuendeleza kwa mioyo yetu yote" Amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amewashukuru Wanafamili wa Marehemu Dkt. Omar Ali Juma kwa uvumilivu na ustahimilivu wao tangu walipoondokewa na mpendwa wao.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Pemba

02 Septemba, 2016.
Rais Magufuli akitazama kikundi cha ngoma baada ya kutua Pemba ambapo pia ameenda kuzulu kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk Omary Ali Juma. Baadaye saa tisa alasiri atafanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Gombani ya Kale, Pemba. Picha na Ikulu

No comments:

Post a Comment

Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina