Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina

Search This Blog

Breaking

Serikali kuja na mpango wa kodi ya nyumba kulipwa mwezi mmoja mmoja

TANGAZA NASI HAPA


2017-11-18

Waziri Mkuu Canada Aijibu Serikali ya Tanzania Sakata la Bombardier Kuzuiliwa Nchini Humo

Wakati katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akiwa nchini Canada kushughulikia suala la ndege ya Bombardier, waziri mkuu wa nchi hiyo, Justin Trudeau amesema hawezi kuingilia uhuru wa mahakama ambayo anaamini itatenda haki.

Hivi karibuni Rais John Magufuli alisema amemwandikia barua waziri huyo mkuu wa Canada ili kujua hatima ya ndege hiyo.

Hata hivyo naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alisema jana kuwa hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sababu waziri mkuu yupo na wao hawajapata taarifa rasmi.

“Lakini kingine naomba utambue kuwa katibu mkuu bado yupo Canada, kwa hiyo mambo mengi mimi sijayapata hadi atakaporudi aje kutu-breaf kilichojiri huko,” alisema Nditiye.

Akizindua uwanja wa ndege mjini Bukoba, Novemba 6, Rais Magufuli alisema amemwandikia barua waziri mkuu wa Canada kumuomba kuachiwa kwa ndege hiyo na amemtuma mwanasheria mkuu wa Serikali, George Masaju kwenda nchini humo kushughulikia suala hilo.

Kwenye barua yake ya majibu ambayo yameripotiwa na gazeti la National Post la nchini humo, waziri mkuu wa Canada Trudeau amesema hana cha kufanya kwa kuwa shauri hilo lipo mahakamani.

“Ni bahati mbaya kwamba suala hili limechelewesha kuwasili kwa ndege hii. Serikali ya Canada haina uwezo wa kuingilia, ila tuna imani mahakama itaamua kwa weledi na haki,” amekaririwa akisema Trudeau katika gazeti hilo.

Ndege hiyo, Bombardier Q400-8 inashikiliwa kwa amri ya mahakama nchini humo kutokana na shauri lililopo kati ya Serikali na kampuni ya Stirling Civil Engineering.

Kampuni hiyo ilikuwa na mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Wazo Hill – Bagamoyo ambao ulivunjika kabla haujakamilika, hivyo ikaamua kukimbilia kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa ambako ilishinda kesi. Baada ya kushinda kampuni hiyo ilipewa kibali cha kukamata mali za Tanzania katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji, Uganda na Canada.

Kwa miezi mitatu sasa, mahakama nchini Canada inaendelea kuishikilia ndege hiyo iliyonunuliwa kwa Dola 32 milioni za Marekani (zaidi ya Sh70.4 bilioni) kwa niaba ya kampuni ya Stirling inayoidai Serikali Dola 28 milioni (zaidi ya Sh61.6 bilioni) ambazo ni thamani ya mkataba uliovunjwa pamoja na riba.

Ndege hiyo ni miongoni mwa zile ambazo Rais Magufuli aliahidi kununua ikiwa ni mikakati ya kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Awali, ndege hiyo litarajiwa kuwasili nchini mwezi Julai, lakini hilo halikufanyika na Agosti 18, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema ndege hiyo imekamatwa nchini Canada na inaweza kupigwa mnada kutokana na deni ambalo Serikali inadaiwa na kampuni hiyo yenye makao yake Montreal, Canada.

Agosti 19, Serikali ilifanya mkutano na wanahabari kukanusha taarifa hizo, lakini ilikiri kuwapo mgogoro na kampuni hiyo.

Aliyekuwa kaimu mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa alisema mgogoro kuhusu ndege hiyo upo na kimsingi umetengenezwa na Watanzania ambao kwa bahati mbaya wameweka masilahi ya kisiasa na ya binafsi mbele zaidi ya masilahi ya Taifa.

Alisema Serikali ilikuwa imeanza majadiliano ya kidiplomasia kwa ajili ya kulimaliza suala hilo. Kwa sasa, ATCL inamiliki ndege mbili mpya aina ya bombardier zilizoingia nchini Septemba 2016, na imeagiza ndege nyingine tatu za aina hiyo na Boeing Dreamliner moja.

Akizungumzia mafanikio ya miaka miwili ya Rais John Magufuli hivi karibuni msemaji mkuu wa Serikali, Hassan Abbasi alisema mpaka Juni mwakani ndege zote zitakuwa zimewasili nchini.

No comments:

Post a Comment

Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina