Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina

Search This Blog

Breaking

Serikali kuja na mpango wa kodi ya nyumba kulipwa mwezi mmoja mmoja

TANGAZA NASI HAPA


2017-12-01

Waziri Mbarawa Atoa Maagizo Mazito Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema anasikitishwa na utendaji wa Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kutofanya maamuzi kwa wakati hali ambayo inachangia malalamiko kuongezeka Bandarini hapo.

Aidha, Mbarawa amesema Serikali inapeleka Naibu Mtendaji Mkuu mpya wa shughuli za Uendeshaji Bandarini hapo kutokana na aliyekuwepo kushindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo.

Profesa Mbarawa amesema hayo leo wakati wa ziara ya kushtukiza aliyoifanya bandarini ikiwa ni siku chache baada ya Rais John Magufuli, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kufanya ziara ya kustukiza na kubaini madudu bandarini hapo.

Ziara ya Waziri Mbarawa ni mwendelezo wa ziara mbalimbali bandarini hapo  kubaini uendeshaji na utendaji wa shughuli zinazotolewa na Mamlaka hiyo.

“Nimelazimika leo kuwaita Watendaji na Bodi ya TPA ili kuwaeleza kasoro zenu  ambapo inaonesha wazi kuwa  asilimia kubwa ya mambo yanayotokea humu  ni  kuwa mnakuwa wazito katika kutoa  maamuzi”, amesema Profesa Mbarawa.

Amesema katika bandari hiyo ipo mizigo ya kahawa ambayo imefika bandarini tangu mwaka 2014 huku kukiwa hakuna sababu za kueleweka za wenye mali kutochukuwa mizigo yao.

Profesa Mbarawa amesema hahitaji wasaidizi ambao wanakaa katika vikao na kulipana posho ila wanapaswa kufanya kazi ya kuangalia shughuli zote za bandari.

“Kama hamtabadilika nitaendelea kuja katika bandari hii ili kuchukua hatua pale ambapo inaonekana kwani haipendezi kila kukicha malalamiko kutokea,” amesisitiza Waziri Mbarawa.

Aidha, Waziri Mbarawa ameitka bodi na menejimenti kuhakikisha kuwa inatatua changamoto iliyopo katika bandari ya kushusha na kupakia mizigo kutoka Zanzibar na kuingia Tanzania Bara ambapo wafanyabiashara wanalalamikia utaratibu unaotumika kuwahudumia.

Amesema haingii akilini kuona mizigo inayotoka au kwenda Zanzibar kutozwa kodi baada ya masaa huku inayotoka nje ya Tanzania ikitozwa baada ya siku saba.

Kuhusu ujio wa Naibu mtendaji Mkuu mpya Mbarawa aliitaka Bodi na menejimenti kumpa ushirikiano ili aweze kutoa matokeo chanya kwenye bandari.

“Tunaleta Naibu Mtendaji Mkuu mpya ambaye atasimamia operesheni, naomba apewe ushirikiano ili kusaidia Serikali huyu ambaye anakaimu tunamuondoa ameshindwa kwenda na kasi yetu,” amefafanua Profesa Mbarawa.

Akizungumza baada ya ziara hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya TPA Ignas Rugaratuka, amesema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa wanaitendea haki nafasi waliyopewa kwa kusimamia mabadiliko ndani ya bandari.
 
Amesema tangu waingie wamekuwa wakipambana kuhakikisha kuwa mapungufu ya TPA yanaisha ambapo wamefanikiwa kurekebisha kwenye utawala kwa kutoa mafunzo kwa watumishi na kuzuia wizi ambao ulikuwa umekithiri.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, amesema kuwa tangu aingie katika mamlaka hiyo wamekuwa wakifanya jitihada za kurekebisha mapungufu na kumuahidi waziri kuwa ataongeza jitihada zaidi.

“Kama ni mabadiliko tumefanya makubwa sana hasa katika utawala na uongozi ila kila anayehusika katika sekta hiyo anapaswa kutoa msaada,” amesema Mkurugenzi Mkuu.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment

Tunakupa habari motomoto na uchambuzi wa kina