MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira
Wilaya ya Maswa (MAUWASA) mkoa wa Simiyu, Lema Jeremiah (50) amefikishwa katika
Mahakama ya Wilaya ya Maswa akikabiliwa na makosa ya wizi wa Sh milioni 108
mali ya serikali.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Nassib Swedy alidai mbele ya
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Tumaini Marwa kuwa mshitakiwa anatuhumiwa
kufanya wizi wa fedha akiwa mtumishi wa Umma.
Swedy alidai Machi 7 mwaka 2014 saa 3:00 asubuhi, Jeremiah akiwa
katika Ofisi za Mamlaka hiyo zilizoko katika kijiji cha Sola wilayani humo
aliiba Sh milioni 108 zikiwa ni mali ya Serikali zilizotolewa na Mwajiri wake
ambaye ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Alisema kosa hilo ni kinyume na Kifungu cha 270 cha kanuni ya
adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.
Hata hivyo, mara baada ya kusomewa shitaka hilo mshitakiwa huyo
alipoulizwa na hakimu Marwa kuhusika nalo, alikana kosa hilo na mwendesha
mashitaka kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe
nyingine ili waendelee na upelelezi na kesi hiyo itatajwa tena Aprili 11 mwaka
huu.
Hakimu Marwa alisema masharti ya dhamana kwa mshitakiwa
anatakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni 50 au hati
ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni 50 na hati hiyo itatakiwa ikaguliwe
kama kweli inafikia kiasi hicho.
Mshitakiwa amekidhi vigezo hivyo na kuachiwa kwa dhamana, lakini
alipotoka mahakamani akashikiliwa na Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU) kwa madai kuwa anahitajika kwa mahojiano zaidi kutokana
na tuhuma nyingine zinazomkabili.
No comments:
Post a Comment