Askari nane wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kigona wakituhumiwa kwa mauaji ya Erick Nilamewa (16) waliyemtuhumu kuwaibia simu moja aina ya Techno na Sh. 6,000.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni Mtaa wa Mabatini Mwanga Manispaa
ya Kigoma/Ujiji.
Wanajeshi hao wakiwa nane, walionekana wakimpiga Nilamewa kwa
mateke, fimbo na kumchoma na pasi tumboni, kifuani na mgongoni, baada ya
kumkamata wakimtuhumu kwa wizi huo.
Mwili wa kijana huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia
maiti katika hospitali ya Mkoa Maweni.
Aidha, Ahamad Mussa, mkazi wa Mabatini eneo la Mwanga Manispaa
ya Kigoma/Ujiji, amelazwa wodi namba 7 katika hospitali ya Mkoa Maweni kwa
matibabu, kutokana na purukushani hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Ferdinard Mtui, alithibitisha
kukamatwa kwa askari hao nane wa JWTZ kwa tuhuma za mauaji ya
kijana huyo na kumjeruhi Mussa (16).
Mtui alisema “Ni
kweli tunawashikilia wanajeshi nane na tunaendelea na upelelezi, na baada ya
uchunguzi tutawapeleka mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.”
Akizungumza kutoka kitandani alikolazwa, Mussa ambaye ni
mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kitwe, alitumiwa
ujumbe wa simu na wanajeshi hao akiwa shuleni ambao walisema kwamba
wanamhitaji.
“Baada ya kutumiwa
ujumbe huo mimi nilimbipu, akanipigia na kujitambulisha kuwa yeye ni afande
Aberi, akasema njoo mara moja nakuhitaji," alisema
Mussa.
"Kwa sababu
tunakaa mtaa mmoja, pia huwa naingiaga kwenye makazi yao wanaponituma vitu
mbalimbali kama sigara, sikuwa na wasiwasi wowote kuhusu wito huo.”
Alisema alipofika alibisha hodi na walimwitikia na kumwambia
akae uani ndipo baada ya muda alitoka Aberi akiwa amevaa kaptura ambaye alianza
kuita wenzake ambao walianza kumsulubu.
“Nilimsikia akiwaita
wenzake wakina afande Mayowa, Ally na wengine nimesahau majina yao lakini jumla
walikuwa wanajeshi nane ambao walikuwa wakinipiga.
"Waliniambia
ninyooshe miguu yangu juu ya ukuta na niliponyoosha walinipiga na ubao na fimbo
ya mianzi kichwani… damu zilianza kutoka.
"Wakachukua maji
wakasafisha, wakapiga tena kichwa nikaanguka chini kisha wakanipiga mateke na
kunichapa na nyaya za umeme huku wakiuliza ilipo simu na Sh 6,000
nilizoiba,” alisema Mussa.
Alisema wakati hali ikizidi kuwa mbaya, "walichukua chupa
ya pombe na kunimiminia" kabla ya kujitokeza mwanamke mmoja wa nyumba ya
jirani anayefahamika kwa jina la mama Hoza ambaye aliwaambia wamwache
"mtoto wa watu maana watamuua bure.
“Mimi sijaiba simu
wala siku ya leo (jana) sijafika kambini hapo.
"Sijaiba wao
wakaendelea kunipiga na kunimwagia maji na kunigalagaza kwenye mchanga wakati
huo damu zinaendelea kuvuja kichwani, ndipo mimi nikawambia naomba niende
nyumbani nikamwambie mama yangu na tulienda na mwanajeshi mmoja na tulipofika
nyumbani tulimkuta mama yangu.
"Mwanajeshi huyo
akasimama nje mimi nikaingia ndani nikapita uani na kukimbia na ndiyo ikawa
pona yangu la sivyo na mimi ningefariki dunia.”
Alisema baada ya yeye kukimbilia ndipo walipomkamata Erick
mtaani na kumpeleka kwenye makazi yao ambako walimpiga na kumtesa hadi
walipoona hali yake kuwa mbaya, walikwenda polisi kuchukua fomu namba 3
(PF3)kwa ajili ya kumpeleka hospitali ya Maweni kwa matibabu, lakini alifariki dunia.
Mama mzazi wa majeruhi huyo, Mwaisala Ahamad (36) alisema
wanajeshi walimuagiza mtoto mmoja kwenda nyumbani kwake kwamba wanamuitaji
mtoto wake na aliwaambia kuwa ameende shuleni.
“Waliniomba namba ya
simu ya mtoto wangu nikawapatia kwasabababu wanajeshi hawa walikuwa na mazoea
na mwanangu,"alisema Mwaisala.
"Nilipowapa
nilienda kwenye shughuli zangu kama kawaida sikuwa na wasiwasi wowote, hawa
tunawajua.
"Wengine wana
nyota moja (luteni nusu) na wengine mbili (luteni) na wengine tatu (kepteni) na
kutokana na vyeo walivyokuwa navyo sikutarajia mtoto wangu yamkute
yaliyomkuta.”
Aliongeza kuwa kama askari hao walihisi kuwa mtoto wake ndiye
aliyeiba simu yao walipaswa kumkamata na kumpeleka kituo cha polisi.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mshumbusi
Edmond alithibitisha kumpokea marehemu Nilamewa akiwa na majerahe kifuani,
tumboni na mgongo lakini akafariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini
hapo.
Mwili wake uko chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya
Mkoa Maweni, alisema.
No comments:
Post a Comment