Polisi mmoja anadaiwa kumpiga risasi dereva daladala, Pistus
Ngowi baada ya kutofautiana kauli.
Tukio hilo lililotokea juzi saa tatu usiku, Kariakoo jijini Dar
es Sallam lilisababisha madereva wenzake wanaofanya wote safari za
Tandika pamoja na wa Temeke kugoma kwa zaidi ya saa tano wakidai kwamba licha
ya kushambuliwa, amebambikiwa kesi katika Kituo cha Polisi cha Msimbazi.
Ilidaiwa kuwa wakiwa katika Mtaa wa Lindi kilipo kituo cha
daladala hizo, polisi huyo aliyetajwa kwa jina moja la Dotto akiwa kwenye
doria, walitofautiana na dereva huyo kisha kumtolea bastola na kumpiga nayo
mkononi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Simon Sirro
alisema jana kuwa awali, alipewa taarifa za askari wake kushambuliwa akiwa
doria na alimpiga risasi dereva huyo kujitetea.
“Huyu askari yupo
mahabusu anahojiwa na polisi ili kubaini chanzo cha tukio hili,”alisema Kamanda Sirro.
Dereva wa daladala aliyeshuhudia tukio hilo, Mateso Elias alidai
kuwa walikuwa madereva 15, waliokuwa wakisubiri abiria ghafla walisikia kelele
za Dotto akimfokea dereva huyo akidai kuwa alitaka kumgonga alipokuwa akiwasili
kituoni hapo.
Alisema ili kuepusha shari, Ngowi alishuka kwenye basi na
kumuomba msamaha akiwa amepiga magoti lakini polisi huyo alikataa kumsamehe.
Alisema kitendo hicho kiliwavuta madereva waliokuwapo hapo ambao
walisogea eneo hilo kujua kilichokuwa kinaendelea: “Ghafla alitoa bastola na kutuamuru wote
tuondoke. Tulipopiga hatua kama hatua tano, alifyatua risasi na kumpiga Ngowi
mkononi na nyingine alipiga hewani.”
Alisema baada ya tukio hilo aliwapigia simu askari wenzake ambao
walifika na kumpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
No comments:
Post a Comment