Serikali imeunda kikosi kazi kinachohusisha taasisi nyeti nchini kuchunguza sakata la kukamatwa kwa raia wawili wa Uholanzi wakiwa katika harakati za kusafirisha tumbili 61 kwenda nchini Albania.
Kikosi hicho kinaundwa na maofisa kutoka ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Kikosi
cha Kupambana na Ujangili.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa
aliwathibitishia wanahabari jana kuundwa kwa kikosi kazi hicho na kwamba,
upelelezi wa sakata hilo umepamba moto.
“Upelelezi ndiyo kwanza
bado mbichi, kwa hiyo siwezi kusema lolote kama lini watuhumiwa watafikishwa
mahakamani kwa sababu upelelezi uko chini ya kikosi kazi hicho,” alisema Mutafungwa.
Juzi saa tano asubuhi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa
Jumanne Maghembe, alitembelea Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Kilimanjaro (Kia) kushuhudia wanyama hao.
Profesa Maghembe alisema kama kila kitu kitakwenda vizuri katika
upelelezi, watuhumiwa wa kosa hilo watafikishwa mahakamani siku ya Jumanne.
Wanyama hao walikamatwa usiku wa kuamkia juzi katika uwanja huo
wakati raia hao, Artem Alik Vardanyian (52) na Eduard Alik Vardanyian (44)
wakiwa katika harakati za kuwasafirisha kwa kutumia ndege kubwa ya mizigo.
Hata hivyo, raia hao wa Uholanzi walikuwa na vibali
vilivyotolewa na Mkurugenzi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Charles
Mulokozi ambaye tayari amesimamishwa kazi kwa kashfa hiyo.
No comments:
Post a Comment