Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe ameagiza mamlaka
zinazohusika kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu
watakaobainika kutafuna fedha za mishahara hewa kabla ya mwezi huu kumalizika.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa agizo hilo juzi kwenye kikao cha
kufahamiana kilichohudhuriwa na wakuu wa wilaya, wakuu wa idara ya sekretarieti
ya mkoa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ofisini kwake.
Katika hotuba yake fupi na ambayo haikuwa na mbwembwe za
kisiasa, alisema uhakiki uliofanyika hivi karibuni mkoani humo ulibainika kuwa
na wafanyakazi hewa wengi, jambo linaloonyesha kuwapo kwa ubadhirifu wa kiwango
cha juu cha fedha za umma.
“Naagiza kila mmoja
wenu akaangalie kwenye taasisi yake iwapo wafanyakazi wanaolipwa mishahara
ndiyo hao waliopo kazini au la. Kuna madai wastaafu, waliohama na hata
watumishi waliokufa mishahara yao bado inalipwa hadi hivi leo,”alisema.
“Iwapo itagundulika
kuwa kuna watu walioshiriki katika ulaji huo wa fedha za umma, wakamatwe mara
moja ifikapo Aprili Mosi, mwaka huu na kufikishwa kunakohusika haraka
iwezekanavyo ili sheria ichukue mkondo wake.”
Mtigumwe aliwakumbusha viongozi hao umuhimu wa watumishi walio
chini yao kufanya kazi kwa uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
“Haiwezekani mtu atoke
kijijini kisha arudi bila kuhudumiwa, lazima kuwahi kazini na kukaa hadi mwisho
wa saa za kazi,” alisema.
Pia, alisisitiza umuhimu wa kila taasisi ya Serikali mkoani humo
kufungua kitabu cha kero za wananchi na kuhakikisha zinaorodheshwa na kuonyesha
hatua halisi iliyofikiwa katika kuzishughulikia.
No comments:
Post a Comment