Mjazi wa Kijiji cha Ikondamoyo, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, Veronica Salehe
(54), aliyeoa wanaume wawili kwa kipindi cha miaka tisa amefariki dunia.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mwenyekiti wa Kitongoji
cha Ikondamoyo, John Maganga, alisema Veronica alifariki dunia wiki iliyopita
mkoani Tabora alikokuwa amekwenda kupatiwa matibabu kwa kaka yake.
Maganga alisema kuwa ndoa hiyo iliwezeshwa na mume mkubwa ambaye
alikubali kuishi na mume mdogo.
Alisema kuwa Veronica ndiye aliyewaoa wanaume wote wawili na
kuishi nao kwa miaka tisa, na kwamba ndiye aliyekuwa na amri kuu katika nyumba
yao.
Aliwataja wanaume hao kuwa ni Paulo Sabuni (62) ambaye ndiye
mume mkubwa na Arcado Mlele (47).
Maganga alisema Veronica na mume wake mkubwa, walifika kijijini
hapo miaka 24 iliyopita wakitokea Kijiji cha Usumbwa, mpakani mwa Chunya na
Tabora.
“Baada ya kufika
kijijini hapa, walianza kujishughulisha na shughuli za kilimo na biashara ya
kuuza pombe za kienyeji aina ya komoni,”alisema Maganga.
Katika uhai wake, Veronica alibahatika kupata watoto wanne, kati
yao wawili wa kike.
Maganga alisema mtoto mdogo wa kiume, ni wa mume mdogo ambaye
ana miaka tisa, anayesoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Ikondamoyo, na
watoto wengine watatu ni wa mume mkubwa.
Kuhusu maisha ya Veronica ya kuishi na wanaume wawili, Maganga
alisema haikuwa siri kijijini hapo kwa sababu walizoeleka kwa wanakijiji.
Alisema mume mdogo alikuwa anaishi kwenye nyumba aliyoachiwa na
marehemu baba yake, lakini alikuwa akishinda kwa mume mkubwa ambako
kulijulikana zaidi kwa jina la ‘nyumba kubwa’.
“Mambo ya kula, kunywa
na mengine, mama alikuwa akiwapangia zamu kama afanyavyo mume mwenye
wake wengi,” alisema Maganga
na kuongeza kuwa wanaume hao walikuwa wanaridhika na kufurahia maisha.
Alisema siku mama akichoka kupika, mume mdogo alikuwa akiingia
jikoni na kuwaandalia chakula watoto na mume mkubwa maji ya kuoga.
No comments:
Post a Comment