
Mkazi wa Gongo la Mboto, Omary Hamis (25) amehukumiwa kifungo
cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka tisa
ambaye ni mlemavu wa kusikia na kuongea.
Hakimu Mkazi, Flora Haule wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala,
alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi wa mashahidi tisa ukiwamo wa daktari
na fomu namba tatu ya polisi (PF3), iliyotolewa mahakamani hapo kama kielelezo
dhidi ya mshtakiwa huyo.
“Mahakama imekukuta na
hatia hivyo inakuhukumu kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na kosa la
kumlawiti mvulana wa miaka tisa ambaye ni mlemavu wa kusikia na kuzungumza, ili
iwe fundisho kwa jamii,” alisema hakimu Haule.
Katika ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, ilidaiwa kuwa mtoto
huyo siku ya tukio alifika kwenye banda la kuonyeshea video ambalo linamilikiwa
na Hamisi saa za jioni, kwa ajili ya kuangalia video, lakini Hamis alimfukuza
kutokana na kutokuwa na pesa ya kiingilio.
Baada ya kumfukuza mtoto huyo aliondoka, lakini baadaye alirudi
bila ya Hamis kuwa na taarifa akakaa ndani ya banda na kisha kupitiwa na
usingizi uliosababisha abaki kwenye banda hilo peke yake hadi usiku.
Hamis alitumia mwanya huo kumlawiti mtoto huyo kwenye jumba bovu
lililopo jirani na ofisi yake hiyo.
Mashahidi waliieleza mahakama kuwa walisikia sauti ya mtu ambayo
ilikuwa haisikiki vizuri akiomba msaada, ndipo waliposogea na kumkuta Hamis
akitekeleza kitendi hicho huku akijua kuwa ni kosa kisheria.
Mashahidi walidai hata walipomkaribia, Hamis aliendelea
kutekeleza kitendo hicho hadi walipolazimika kumpiga mateke. Hamis alikiri kuwa
siku hiyo watoto walifika kwenye banda lake hilo.
Wakili wa Serikali, Ester Kyara aliiomba mahakama hiyo kutoa
adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa wote wanaotumia mabanda ya
kuonyesha video kufanya ukatili kwa watoto.
Katika utetezi wake, Hamisi alisema ana familia inayomtegemea
hivyo apunguziwe adhabu, maombi ambayo yalitupiliwa mbali na mahakama hiyo na
kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Hamisi anadaiwa kutenda kosa hilo Agost 26, 2014 eneo la Gongo
la Mboto.
No comments:
Post a Comment