Ofisi ya Elimu wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani imelazimika
kuwapa likizo walimu saba wa Shule ya Msingi Mingwata ili kuwajenga
kisaikolojia baada ya kukithiri kwa matukio ya kishirikina yanayowakumba katika
shule hiyo.
Walimu hao wanakumbana na matukio ya ajabu ikiwamo kujikuta
uchi, kupigwa fimbo na mtu asiyeonekana na kulazwa nje ya nyumba zao.
Mmoja wa walimu walioathirika na matukio hayo, Emmanuel Shaaban
alisema yeye na familia yake hawana raha kutokana na matukio hayo kwa kuwa
usiku huvuliwa nguo na kujikuta wamelazwa sehemu nyingine, huku wakiwa
wamechanjwa kwa wembe mwili mzima.
“Tarehe 26 mwezi wa
pili, siku ya Alhamisi sitaisahau kabisa. Ndiyo siku ambayo nilikatwa viwembe
mwili mzima na hali yangu ilikuwa mbaya, niliishiwa nguvu na mwili ukawa na
ganzi na nilipokwenda hospitali niliambiwa sina ugonjwa,” alisema Shaaban.
Alisema alipotoka hospitali alikwenda kijijini kwao mkoani
Mwanza na huko aliendelea kuwa na hali mbaya kutokana na kuzimia mara kwa mara kwa
sababu ya maumivu ya kichwa hadi alipotibiwa kienyeji.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mikidadi Mbelwa alisema awali
alikuwa akiona vituko usiku na mchana, lakini alivumilia huku akitunza siri
bila kuwaeleza wenzake ili asiwakatishe tamaa.
Mbelwa alisema baadhi ya matukio aliyokutana nayo ni kuvuliwa
nguo usiku, kulazwa eneo jingine, kuchapwa viboko, kumwagiwa damu kwenye korido
ya nyumba, kuchanjwa kwa wembe, kuzungukwa na nyoka mwilini, kuona mtu na kisha
anapotea na kutupwa kwenye mashimo.
Mzazi wa watoto wanaosoma katika shule hiyo, Asha Kondo alikiri
kuwapo kwa matukio ya watoto kuugua na kuanguka hadi uongozi wa kijiji
ulipopeleka mganga wa kienyeji kutoa kinachodaiwa ni uchawi.
Mratibu wa Elimu wa Kata ya Marui, Damaru Charles alisema
amekuwa akipokea malalamiko hayo na kuyawasilisha ngazi za juu.
Ofisa Elimu Msingi wilayani hapa, Aurelia Rwenza alisema tatizo
hilo linawapa shida walimu na kurudisha nyuma maendeleo ya elimu katika sehemu
hiyo.
“Kwa kweli walimu
wameathirika, hivi sasa tunatakiwa kuwajenga kisaikolojia,” alisema.
No comments:
Post a Comment