Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemhukumu Ally Rashid maarufu kwa jina la Ally Mwizi kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti msichana mwenye umri wa miaka 25, makaburini.
Hukumu hiyo iliyovuta hisia za watu wengi wa Manispaa ya Mpanda ilitolewa jana na Hakimu wa mahakama hiyo, Chiganga Ntengwa baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka pasipo kutia shaka, ukiongozwa na Mwanasheria wa Serikali wa Mkoa wa Katavi, Jamila Mziray.
Awali Mwendesha Mashtaka Mziray alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 17, mwaka huu, saa 2:00 usiku katika makaburi ya Kashaulili yaliyoko katika Mtaa wa Kotazi, Manispaa ya Mpanda.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa kabla ya kutenda kosa hilo alimfuata msichana huyo ambaye alikuwa ameibiwa vitu vyake vya ndani ya nyumba ambapo alimdanganya kuwa ana uwezo wa kumsaidia kuvipata vitu vyote alivyoibiwa.
Mziray alidai kuwa baada ya msichana huyo kuahidiwa na mshtakiwa kuwa vitu vyake alivyoibiwa vitapatikana alimlipa mshtakiwa Sh 30,000 ili akamwoneshe vitu vyake alivyoibiwa.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa siku hiyo ya tukio mshtakiwa alimpigia simu msichana huyo saa 2:00 usiku akimtaka waonane ili akamwonesha vitu vyake vilivyoibiwa.
Mziray alieleza mshtakiwa alikwenda nyumbani kwa msichana huyo na wakaongozana hadi kwenye makaburi ya Kashaulili ambako alidai ndiko vilipo vitu vilivyoibwa lakini ghafla mshtakiwa alimpiga ngwala msichana huyo na kumbaka na kumlawiti huku akimtishia maisha iwapo akijaribu kupiga kelele.
“Baada ya kumtendea unyama msichana huyo, mshtakiwa alimwomba dada huyo waende kwenye nyumba ya kulala wageni inayoitwa Kingi Paris ili wakaendelee kufanya mapenzi zaidi kwa kile alichodai kuwa nyumba hiyo ya wageni inafaa zaidi kufanyia tendo la ndoa kuliko juu ya kaburi,” alidai.
No comments:
Post a Comment