WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa miezi mitatu kwa Bodi mpya ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kusuka upya uongozi uliopo ili kuweza kuleta ufanisi wa utendaji kazi wa Shirika hilo.
Akizungumza jijini Dar es salaam mara baada ya kuitambulisha Bodi hiyo, Waziri Mbarawa amesema kuwa Uteuzi wa Bodi hiyo utasimamia kuleta tija na ufanisi wa shirika hilo ambalo kwa kipindi kirefu lilikuwa na changamoto nyingi.
“Nataka kuona mabadiliko makubwa kuanzia kwenye Menejimenti hadi uongozi wa chini, hakikisheni mnaweka uongozi amabao utafuata maadili, utakuwa na ufanisi, ubunifu na kasi katika utendaji kazi” amesema Profesa Mbarawa.
Aidha, ameitaka Bodi hiyo kusimamia na kuboresha mpango wa kibiashara wa usafirishaji (Business Plan) katika Shirika hilo ili kuweza kumudu soko la ushindani na kuweza kuongeza mapato ya Shirika hilo.
“Kama mnavyojua usafiri wa anga una ushindani mkubwa, hivyo ili Serikali iweze kupata faida katika biashara hii ni lazima tuboreshe mpango wa kibiashara unaoendana na wakati”, amesisistiza Waziri Mbarawa.
Profesa Mbarawa ameitaka Bodi hiyo kuipa ATCL mifumo imara, makini na mahiri ili kuweza kutatua changamoto zinazoikabili Shirika hilo ikwemo wizi wa mafuta ya ndege na upotevu wa mapato.
Ili kupima ufanisi wa utendaji wa Shirika hilo Profesa Mbarawa ameitaka Bodi hiyo kuandaa mkataba kwa kila mfanyakazi kuanzia ngazi ya juu hadi chini.
Katika hatua nyingine Waziri Mbarawa amesema kuwa Serikali ina mpango wa kununua ndege mbili mpya aina ya Jet ifikapo mwaka 2017 kwa lengo la kuboresha sekta ya usafirishaji wa anga nchini.
Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, ameitaka Bodi hiyo kutumia fursa walioipata katika kufanya kazi vizuri ili kufufua shirika hilo na kuwapatia watanzania huduma sahihi na bora za usafirishaji.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Emmanuel Korosso, ameahidi kushirikiana na wajumbe wa bodi yake katika kutekeleza maelekezo ya Waziri haraka iwezekanavyo ikiwemo kubadilisha menejimenti ya shirika hilo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment