Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amezindua mifumo miwili ya kielektroniki
itakayosaidia kuandaa bajeti kwenye ngazi ya serikali za Mitaa huku
akitoa onyo kali kwamba mifumo hiyo isitumike kukwamisha shughuli au
utaratibu wa kazi za serikali .
Waziri
Majaliwa amezindua mifumo hiyo jana mjini Dodoma na kusema lengo la
mifumo hiyo mipya ni kuongeza uwajibikaji na ufanisi na kamwe isiwe
kikwazo katika utoaji wa huduma kwa jamii.
"Napenda
kutumia fursa hii kuwafahamisha viongozi na watendaji pamoja na
wananchi wote kwamba, lengo la matumizi ya mifumo ya TEHAMA ni kuongeza
uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za
serikali na isitumike kukwamisha shughuli au utaratibu wa kazi za
serikali. Ni muhimu mifumo hiyo itumike kwa ufasaha ili kuleta tija
inayotarajiwa na kila muhusika kwa ahakikishe anailinda, anaitunza na
kuitumia mifumo hiyo ili iweze kudumu na kuwa endelevu kwa manufaa ya
taifa", alisema Waziri Majaliwa.
Pia
Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa mikoa na Halmashauri na vituo vya
kutoa huduma za elimu na afya kutoa taarifa ya mapato na matumizi kwa
mamlaka zinazohusika kwa wakati.
"Ngazi
zote za mamlaka za serikali za mitaa zitoe taarifa za mapato na
matumizi kwa wananchi wanaowahudumia kupitia mikutano, mbao za
matangazo, tovuti, vyombo vya habari na njia nyinginezo", alisisitiza Waziri Majaliwa.
Waziri
Mkuu alisema kwa sasa serikali haitarajii kuona kituo chochote cha
kutoa huduma za elimu na afya kilichopo chini ya Halmashauri kinakuwa na
matumizi yasiyozingatia taratibu na kanuni za fedha za umma.
"Hatutarajii
kuona viongozi wa mikoa na Halmashauri wakibadilisha matumizi ya fedha
bila kuwasiliana na Mamlaka husika. Matumizi ya fedha yafanyike
kutegemea chanzo cha fedha kilichopokelewa kwa wakati na kwa mujibu wa
bajeti iliyotengwa kwa mwaka husika.
"Serikali
ina matarajio makubwa na mifumo hii, na nitapenda Ofisi ya Rais -
TAMISEMI na Ofisi yangu zipate taarifa zote za mipango, bajeti pamoja na
taarifa za fedha zinazopelekwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa
wakati na zikiwa katika ubora wa hali ya juu." alisema Waziri Majaliwa
Mifumo
iliyozinduliwa jana ni mfumo wa kupanga mipango, kuandaa bajeti na
kutolea taarifa za hatua za utekelezaji wa bajeti (Planning, Budgeting
and Reporting System- PlanRep) pamoja na mfumo wa kufanya malipo na
kutoa taarifa za fedha ambazo zimetumwa kwenye vituo vya kutoa huduma
(Facility Financial Accounting and Reporting System-FFARS).
No comments:
Post a Comment