Rais
John Magufuli amesema hakubomoa jengo la Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) lililopo Ubungo alipokuwa waziri wa ujenzi kwa kuwa aliogopa
kufukuzwa kazi.
Rais
Magufuli amesema hayo leo Jumamosi Novemba 25,2017 alipozindua
Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbili (Muhas), kampasi ya Mloganzila.
Akizungumza
mbele ya waziri mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mizengo Pinda
aliyehudhuria uzinduzi huo, Magufuli amesema wakati huo aliogopa baada
ya kuzuiwa na waziri mkuu huyo, lakini sasa yeye ndiye Rais hakuna wa
kumzuia.
Akizungumzia
ubomoaji unaoendelea sasa amesema, “Nilishatoa maagizo, najua Mizengo
Pinda kwenye hili alinipinga wakati ule, lakini najua leo hawezi
akanipinga kwa sababu mimi ndiye Rais. Wakati ule nilikuwa waziri wake,
ndiyo maana nilinyamaza nilijua ninaweza nikafukuzwa, hutakiwi kumpinga
mkubwa.”
“Hilo
jengo la Tanesco, narudia kama itakuwa ni kubomoa nusu, no problem
(hakuna tatizo); kama ni lote hakuna tatizo, pamoja na jengo la wizara
ya maji. Najua katibu mkuu wa wizara ya maji yupo hapa ananiangalia,
wakaanze kulitoa eneo lililopo kwenye hifadhi ya barabara,” amesema.
Machi
6, 2011 akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara mjini Chato,
mkoani Kagera, Pinda ambaye alisifia utendaji wa Dk Magufuli alimwagiza
kusimamisha ubomoaji maeneo kadhaa yaliyokuwa kwenye hifadhi ya barabara
likiwemo jengo la Tanesco hadi Serikali itakapotoa kauli nyingine
kuhusu hilo.
Pinda
alikuwa akizungumzia hatua ya Dk Magufuli aliyekuwa amewaagiza wananchi
waliojenga nyumba ndani ya hifadhi ya barabara kuanza kubomoa nyumba
hizo na wasitarajie kulipwa fidia.
Pinda
wakati huo akiwa waziri mkuu alisema spidi (kasi) ya Magufuli ilikuwa
kubwa hivyo alimuagiza kusimamisha ubomoaji huo hadi suala hilo
litakapojadiliwa na Baraza la Mawaziri.
Pinda,
ambaye alikuwa waziri mkuu kuanzia 2008 baada ya kujiuzulu kwa Edward
Lowassa alisimamisha ubomoaji huo ili kutoa nafasi kwa Serikali
kujipanga upya.
Alisema Serikali inamuamini Magufuli kuwa kiongozi mwenye uwezo na ndio maana ilimpa nafasi akawabane makandarasi wazembe.
Dk
Magufuli akiwasilisha bajeti bungeni mwaka 2012/13, alizungumzia
ubomoaji akisema siasa iachwe akisisitiza sheria zimepitishwa ikiwamo
Sheria namba 13 ya mwaka 2007 na ya hifadhi ya barabara iliyoanza tangu
mwaka 1932.
Alizungumzia
jengo la Tanesco alisema liko kwenye hifadhi ya barabara na kwamba hata
kama asipolibomoa yeye kuna siku litabomolewa vinginevyo sheria
ibadilishwe.
Novemba
15 akitokea Chato alipokwenda kwa mapumziko baada ya ziara ya Uganda,
Magufuli alimuagiza wakala wa barabara nchini (Tanroads) kuweka alama ya
X katika jengo la Tanesco na Wizara ya Maji, sehemu zilizo katika
hifadhi ya barabara.
No comments:
Post a Comment