Ukawa wamedai wafuasi wake 38 wapo rumande za polisi kwa muda mrefu, huku Chadema ikisema Jumanne ijayo itawasilisha ombi Mahakama Kuu kutaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini aitwe kueleza sababu za kushindwa kuwafikisha watuhumiwa mahakamani.
Jana, Chadema wametoa taarifa kwenye vyombo vya habari wakisema Jeshi la Polisi linawashikilia wanachama wake 10 kwa zaidi ya wiki mbili sasa, wakati CUF ilidai wanachma wake 28 wako kwenye mahabusu za polisi kwa muda mrefu.
Mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwaambia waandishi wa habari kuwa Jumanne watawasilisha ombi Mahakama Kuu kutaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Ernest Mangu aitwe mahakamani kueleza sababu za kutowafikisha mahakamani watuhumiwa hao.
Lakini, Mkurugenzi wa Upelelelzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani amepinga madai ya watu kukamatwa kwa sababu za kisiasa pia alivitaka vyama hivyo kwenda vituo vya polisi kuangalia makosa yaliyotendwa kama yanahusiana na uanachama wa vyama vyao.
Lissu amesema watu hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika mikoa mbalimbali ukiwamo wa Songwe na walisafirishwa hadi Dar es Salaam na kuwekwa mahabusu katika vituo vya polisi Kanda Maalamu ya Dar es Salaam.
“Ikifika Jumanne ijayo kama watu hawa 10 hawatapelekwa mahakamani wala polisi kuwaachia kwa dhamana, tunakwenda kufungua maombi ya kuwaita IGP au DCI kwa sababu Mahakama Kuu ina mamlaka ya kuamuru mamlaka yoyote ya Serikali inayoshikilia mtu, kumwita mkuu wa mamlaka kueleza kwanini inamshikilia mtuhumiwa kwa muda uliozidi kisheria.
“IGP na wasaidizi wake akiwamo DCI, wataieleza Mahakama Kuu kwanini wanashikilia watu hao kwa muda mrefu. Kati ya watuhumiwa hao, wawili wapo kituo cha Kanda Maalumu (Central Police) na nane wapo Oysterbay,” alisema Lissu.
Wanaodaiwa kushikiliwa Kanda Maalumu waliotajwa na Idara ya Habari ya Chadema ni Ben Nzogu na Mussa Sikabwe wakati wanaodaiwa kuwa Oysterbay ni Aristotle Mgasi, Hosia Mbuba na Ignasia Mzenga,
Wengine ni Mdude Nyangali, Shakira Abdallah Makame, Dk David Nicas, Juma Salum na Suleiman Said.
Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema wapo katika hatua za mwisho za kuandaa hati ya kupeleka Mahakama Kuu endapo watu hao hawatapewa dhamana na polisi au kupelekwa mahakamani.
Kwa mujibu wa Lissu, watu hao wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kutoa na kusambaza katika mitandao ya kijamii maneno yasiyomfaa Rais John Magufuli, huku wengine wakituhumiwa kwa kosa la studio yao kutengeneza wimbo wenye uchochezi.
“Hawa ni watu wadogo sana, ndiyo maana wanafanyiwa hivi. Ingetokea kwangu mimi au Mbowe (Freeman), mngeona kesho yake tumepelekwa mahakamani. Jamani mahabusu siyo kuzuri, niulizeni mimi,” amesema Lissu.
Mwanasheria huyo ameongeza, “sheria inasema mtu anatakiwa ashikiliwe na polisi kwa saa 24 na baada ya hapo anapelekwa mahakamani isipokuwa akikamatwa siku zisizo za mahakama, lakini kwao hawa wenzetu ni kinyume na wanazidi kuteseka,” alisema Lissu.
Lissu alidai alikutana na watuhumiwa hao wakiwa katika mahabusu na alielezwa mateso wanayoyapata baada ya kupelekwa sehemu fulani ambayo walikwenda kushughulikiwa na kikosi kazi kinachojumuisha vyombo vya ulinzi.
“Huwa wanachukuliwa kutoka mahabusu usiku na kupelekwa mikocheni kwenye kituo cha mateso. Wanavuliwa nguo na wanapigwa hadi kuvuja damu. Wanawekwa katika vituo vya polisi zaidi ya wiki mbili bila kupelekwa mahakamani kwa sababu tu ya tuhuma.
“Katiba ya nchi, Ibara ya 13, ibara ndogo ya sita inapiga marufuku mtu kuteswa, kudhalilishwa na kuwapa adhabu ya kinyama. Lakini, Tanzania ya leo kuna sehemu imeandaliwa kwa ajili ya kuwatesa watu,” alisema Lissu.
Mbali na watu hao 10, Lissu alisema amepata taarifa zisizo rasmi kuwa watu wengine 73 ambao hawajafahamika kutoka mikoani, nao wanashikiliwa kwa makosa mbalimbali ikiwamo kutoa maoni ambayo hayampendezi kiongozi wa nchi.
“Wakifika hapa Dar, mwenyewe mamlaka ya kuwashughulikia ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), siyo mkuu wa upelelezi wala kamanda wa mkoa husika.
“Sitaacha kusema ukweli, nitaendelea kusema kutokana na mambo mabaya yanayofanyika katika nchi hii,” alisema Lissu.
Katika hatua nyingine, Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF, Mbarara Maharagande amesema tatizo kama hilo pia linawakabili wanachama wa chama hicho, lakini hawatarudi nyuma kuwapigania.
Amesema Tanzania Bara wapo wanachama 10 kutoka mikoa ya Tanga na Mtwara ambao wanashikiliwa na polisi kwa muda mrefu kwa tuhuma za kisiasa, huku Pemba na Unguja wakiwa 18 wanaotuhumiwa kukata mikarafuu.
“Viongozi wetu wa ngazi husika bado wanapambana na suala hili. Tutahakikisha wanapelekwa mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake,” alisema Maharagande.
Akizungumzia madai hayo, DCI Athuman Diwani amesema polisi katika utendaji kazi inaangalia kosa alilolifanya mhalifu na kwamba hawaangalii kilichofanywa na mwanachama wa chama fulani.
Alipoulizwa sababu za kuchelewa kuwapeleka watuhumiwa hao mahakamani, DCI alimtaka Lissu awasiliane na wapelelezi kujua sababu za kuchelewa kwa kuwa kuna sababu nyingi za mtuhumiwa kupelekwa mahakamani.
“Mojawapo ya sababu ni mahojiano yanayoyafanyika kati ya mtuhumiwa na polisi kuhusiana na makosa aliyoyatenda,” alisema.
Mkurugenzi huyo aliongeza, “Lakini nimesikia kuwa wanakwenda mahakamani, waache waende kwa sababu ni haki ya kila Mtanzania,”alisema Athuman.
Hata hivyo, alisema jana kuna watuhumiwa wengi walipelekwa mahakamani, hivyo huenda watu anaowasema Lissu wakawa ni miongoni mwao.
Pia, aliwataka viongozi wa CUF kwenda polisi na kueleza kuwa watu waliokamatwa ni watu wao, ili jeshi hilo liangalie uhusiano wa makosa na uanachama wao.
No comments:
Post a Comment