Hatimaye,
uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) umekanusha juu ya taarifa
ambazo zilikuwa zinasambaa zikiwahusu vigogo wa shirikisho hilo
wakiongozwa na rais wao, Wallace Karia kujilipa posho ya kiwango cha
juu.
Hivi karibuni kulisambaa taarifa mitandaoni juu ya vigogo hao wa TFF kujilipa fedha nyingi.
Kumbuka
viongozi wa kuchaguliwa TFF hawapati mishahara, badala yake wanalipwa
posho, sasa ilielezwa kwamba Karia analipwa Sh milioni sita, makamu wake
Sh milioni tano huku wajumbe wa Kamati ya Utendaji wakilipwa milioni
moja kwa kila mwezi.
Kaimu
Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, amesema suala hilo halina ukweli na
kudai kuwa Karia alikataa kulipwa na kusisitiza posho yake ipelekwe
katika masuala mingine ya kimpira kwa kuwa yeye ni muajiriwa serikalini
na analipwa mshahara huko.
“Hizo taarifa hazina ukweli wowote kwa sababu viongozi wa hapa hakuna ambaye anachukua kiasi hicho cha fedha.
“Hata
kwenye suala la wajumbe, nao hakuna ambaye anapokea shilingi milioni
moja kwa mwezi kama inavyosemekana badala yake tunatoa shilingi milioni
moja na nusu kwa miezi mitatu tena kwa yule ambaye anachakarika na
tunaona juhudi zake kwa kupitia ripoti ambazo anawasilisha kwenye vikao.
“Lakini
kwa sababu jambo hilo limechafua sura ya taasisi yetu tuna mpango wa
kuwafungulia kesi ya makosa ya kimtandao wale wote ambao wamehusika
kwenye suala hilo na tayari tuna majina 10 ya watu ambao tutaanza nao,”
alisema Kidau.
Pamoja
na TFF kuamua kulitolea ufafanuzi suala hilo, bado inaonekana haukuwa
mjadala mpana hasa nje ya mitandao na huenda waliamua kuwahi mapema ili
kumaliza mjadala.
WARAKA WA TUHUMA UNAZOSAMBAZWA NI HUU;
“KAMATI TENDAJI YA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF) KUTUMIA MILIONI 438 KWA MWAKA KUJILIPA POSHO.
Tarehe
28/10/2017 Kamati ya Utendaji ya TFF, ilifanya Kikao katika Hoteli ya
SEA SCAPE Kunduchi Beach jijiji Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo
mengine ilipitisha azimio la Wajumbe wa Kamati hiyo kuanza kulipwa
posho ya kila mwezi kwa mchanganuo ufuatao:
1. Rais wa TFF Tsh.Mil.6 kwa mwezi sawa na Mil.72 kwa Mwaka.
2. Makamu wa Rais wa TFF, Tsh. mil. 5 kwa mwezi sawa na Mil.60 kwa mwaka.
3.
Wajumbe 20 wa Kamati ya Utendaji kila mmoja Tsh. Mil. 1 kwa mwezi sawa
na mil.12 kwa mwaka , kwa wajumbe 20 ni Tsh. Mil. 240 kwa mwaka.
NB: Posho hizi ni mpya na hazijawahi kuwepo katika shirikisho hilo katika uongozi uliopita.
Aidha
Posho za kila kikao zimepanda kutoka Tsh. 300, 000/= uongozi uliopita
hadi laki tano (500,000/) uongozi wa sasa kwa kila mjumbe, kwa mwaka
kuna vikao vya kawaida visivyopungua sita, kwa Wajumbe wote 22 kwa
mwaka itakuwa mil.66.
Kwa
mchanganuo huo, Gharama za Posho tu kwa mwaka kwa Wajumbe wa Kamati ya
Utendaji tu ni milioni mia nne thelathini na nane (mil.438). Bado posho
za vikao vya dharura, posho za watumishi wengine n.k
Moja
ya changamoto za maendeleo ya Mpira wa Miguu Tanzania ni Ukosefu wa
fedha. Timu zetu za taifa zinashindwa kukaa kambini, Waamuzi wanakosa
Mafunzo, viwanja vya michezo vinashindwa kuboreshwa, vilabu vya michezo
havisaidiwi na mambo mengine chungu nzima hayafanyiki sababu ya ukosefu
wa fedha, leo hii EXCOM inakwenda kujifungia Sea ESCAPE na kuidhinisha
mil. 438 kwa ajili kujilipa posho!
Kwa
mwendo huu tusitegemee maendeleo katika soka Tanzania. Rais wa TFF,
WALES KARIA na Makamu wake, MICHAEL WAMBURA wanapaswa kujitathmini
upya,”.
No comments:
Post a Comment