Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoa wa Singida Bi Lucy Mayenga. |
Wakati Taifa likisubiri uteuzi wa wakuu
wa wilaya huku wanaoshikilia nafasi hizo wakiwa katika chekeche kwa kuzingatia
vigezo vitano, Mkuu wa Wilaya Iramba, mkoani Singida, Lucy Mayenga amemuomba
Rais John Magufuli asimjumuishe kwenye orodha ya wakuu hao anayotarajia
kuitangaza wakati wowote.
Rais Magufuli ameweka bayana vigezo
atakavyotumia kufanya uteuzi wa wakuu hao wa wilaya ambavyo ni pamoja na suala
la migogoro ya ardhi, tatizo la elimu hasa upungufu wa madawati, njaa na
mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu alivyovitangaza wakati akizungumza na wazee
wa Dar es Salaam na katika uteuzi wa wakuu wa mikoa, alizungumzia pia suala la
wafanyakazi hewa ambao wamekuwa wakilipwa mishahara bila ya wahusika kuchukua
hatua kudhibiti.
Akizungumza kwenye kikao cha UWT, Mkoa
wa Shinyanga mwishoni mwa wiki, Mayenga ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalumu
alisema aliwasilisha ombi hilo binafsi kwa Rais Magufuli ili apate fursa ya
kusimamia biashara zake alizosema zinazodorora kutokana na kubanwa na majukumu
ya ukuu wa wilaya.
“Pamoja
na ukuu wa wilaya, mimi pia ni mbunge na wakati huohuo ni mfanyabiashara; haya
ni majukumu mengi kutekelezwa na mtu mmoja kwa wakati moja,”alisema Mayenga
Aliwaambia wajumbe waliohudhuria mkutano
huo uliofanyika katika Kata ya Nyamilangano, wilayani Ushetu kuwa biashara zake
nyingi zilizopo mkoani Shinyanga zimedorora kutokana na kukosa usimamizi wake.
“Ombi
hili nililitoa binafsi kwa Waziri Mkuu ambaye alinishauri kusubiri uteuzi;
isitafsiriwe kwamba nimeogopa kasi ya utendaji ya Serikali ya Awamu ya
Tano.Hapana! Nimeona ni vyema nibaki na ubunge na biashara zangu,” alisema Mayenga ambaye
kitaaluma ni mwandishi wa habari.
Baadhi ya wanachama wa UWT waliohudhuria
mkutano huo walimpongeza kwa uamuzi huo wakisema unapaswa kuigwa na viongozi
wengine wenye majukumu mengi kwa kuachia watu wengine nafasi za kutumikia umma
badala ya kung’ang’ania nafasi zote.
“Nampongeza
Mheshimiwa Mayenga kwa uamuzi wake wa kuomba asiteuliwe tena kwenye nafasi ya
ukuu wa wilaya kwa sababu itatoa fursa kwa watu wengine kutumikia nafasi hiyo,” alisema Selina
Mkula.
Katika mkutano huo ambao Mbunge wa
Ushetu, Elias Kwandikwa alitoa msaada wa mifuko 60 ya saruji kwa ajili ya
ujenzi wa madarasa katika shule za msingi Nyamilangano na Mitonga pamoja na
Shule ya Sekondari Kisuke, wanachama wapya 55 walijiunga na UWT.
Mbunge
huyo pia aliahidi kutoa vyerehani 20 kwa makatibu kata wa UWT ili kusaidia harakati
za maendeleo ya wananchi kwa kuanzisha vikundi vya kiuchumi katika kata zao.
No comments:
Post a Comment