watoto hao wanaosoma
darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya Msaranga Manispaa ya Moshi
Watoto wanne wa kike wenye umri wa miaka
minane wamebainika kunajisiwa kwa karibu mwaka mzima huku vijana wawili
wanaowafanyia vitendo hivyo wakiwalipa Sh500 kila mmoja.
Habari zinasema watoto hao wanaosoma darasa la
tatu katika Shule ya Msingi ya Msaranga Manispaa ya Moshi, wamekuwa
wakienda kufanyiwa vitendo hivyo asubuhi kabla ya kuingia darasani.
Uchunguzi wa madaktari wa hospitali ya rufaa ya
Mkoa Kilimanjaro ya Mawenzi umethibitisha watoto hao kuingiliwa kwa kunajisiwa
na kuambukizwa magonjwa ya zinaa.
Watoto hao wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo
kati ya saa 12.30 na saa 1.30 asubuhi na baadaye hutakiwa kurudi saa nne wakati
wa mapumziko kuchukua Sh500 kama malipo ya ujira wa kazi hiyo.
Mkazi mmoja wa Msaranga ambaye hakutaka jina lake
kutajwa, alishuku mwenendo usio wa kawaida wa mjukuu wake ambaye ni miongoni
mwa watoto hao.
“Ilikuwa kati ya saa 12.30 au saa 1.00
asubuhi nilikuwa natoka misa ya asubuhi nikakutana naye na wenzake wanavuka
barabara kwenda upande tofauti na ilipo shule,” alisema mzee huyo.
“Nilipomuuliza unakwenda wapi akasema mwalimu
amewatuma madekio, lakini nikamuona anatetemeka. Nikamuamuru arudi shule
mara moja. Mie nikaendelea na safari yangu lakini roho ikakataa.”
Mzee huyo alisema saa mbili asubuhi siku
hiyohiyo, alikwenda shuleni kukutana na mwalimu mkuu lakini alikutana na
mwalimu wa zamu na kumueleza shaka yake.
Kwa mujibu wa mzee huyo, mwalimu aliahidi
kuchunguza jambo hilo, lakini siku hiyo mjukuu wake aliporudi nyumbani
alimuuliza na baada ya kumchapa kidogo akaeleza kila kitu.
Siku iliyofuata mzee huyo alirudi shuleni na
kumueleza mwalimu mkuu taarifa zile naye aliita walimu wenzake na kumuita mtoto
huyo na kumuuliza kama ni kweli alichoeleza babu yake.
“Mwalimu mkuu akamwambia usiposema ukweli
nitakuadhibu, ndipo akasema huwa wanakwenda kwa wavulana fulani kufanya hayo
mambo na akawataja wenzake watatu anaokwenda nao,” alisema.
Mlezi huyo alidai mbele ya walimu alieleza kuwa
huwa wanakwenda huko asubuhi na kufanyiwa vitendo hivyo kwa zamu katika chumba
kimoja halafu hutakiwa kurudi saa nne asubuhi kuchukua Sh500.
“Watoto wawili akiwamo huyu mjukuu wangu walikiri
na kuwataja kwa majina vijana na kutueleza fulani huwa anatufanya mbele na
fulani anatufanya nyuma. Wawili waligoma kueleza,” alisema.
“Wametwambia saa nne wakati wa mapumziko ndiyo
wanakwenda kuchukua hiyo 500 kila mmoja halafu siku nyingine hurudi saa nane
mchana,” alisema.
Mtoto huyo alipohojiwa na mwandishi wetu alitoa
maelezo yanayofanana na ya babu yake na kuwataja majina vijana hao.
Alhamisi iliyopita, majirani walihamasishana
kwenda kwenye nyumba husika eneo la Lombeta, umbali wa mita 800 kutoka shuleni
hapo, lakini kabla ya kufanya hivyo walimpigia simu mwenyekiti wa mtaa ambaye
aliwashauri waende polisi.
“Tulipofika Polisi Majengo tukapewa PF3 (fomu ya
polisi) tukaenda na wale watoto wawili hadi kwa daktari Mawenzi na baada ya
kuwapima alishtuka sana,” alisema mmoja wa majirani hao, Lilian Kisanga.
Kisanga alisema daktari aliwashauri warudi siku
inayofuata kwa ajili ya watoto kupimwa kama wameambukizwa magonjwa ya zinaa na
vipimo vilithibitisha watoto hao kuambukizwa.
“Ijumaa tulikwenda na polisi kwenye ile nyumba
tukafanikiwa kumkamata kijana mmoja ambaye watoto wanamtambua kwa sura na
jina,” alisema Lilian.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad
Mutafungwa alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa mmoja wa tukio hilo.
“Ni kweli kuna shauri hilo limefunguliwa na
tayari tumemkamata mmoja wa watuhumiwa na tunaendelea kumtafuta mwingine
anayetajwa na watoto hao,” alisema.
Mutafungwa alisema kutokana na uzito wa kosa hilo
ambalo likithibitika mahakamani adhabu yake ni kifungo cha maisha, ameagiza
dhamana ya mtuhumiwa izuiliwe kwa sasa.
“Ni matukio mabaya na machafu ambayo mtu
ukiyasikia yanaumiza sana. Tayari nimeagiza jalada lihamishwe kutoka Majengo
lipelekwe Dawati la Jinsia,” alisema Mtanfungwa na kuongeza:
“Tunawaomba wananchi wenye taarifa za mahali
alipo mtuhumiwa wa pili watuletee ili akamatwe na yeye mwenyewe huko aliko
ajisalimishe.”
Taasisi mbalimbali za kutetea haki za wanawake na
watoto mkoani Kilimanjaro zimeapa kulivalia njuga suala hilo na leo watapiga
kambi kituo kikuu cha kati cha Polisi kufuatilia sakata hilo.
Mkurugenzi wa taasisi ya Kilimanjaro Women
Information Exchange and Consultancy Organisation (Kwieco), Elizabeth Minde
aliwataka polisi kuchunguza tukio hilo kwa uzito unaostahili.
“Tunataka uchunguzi wa kina ufanyike ni tukio
baya ambalo limetushtua sisi kama wazazi. Uko nyumbani unaamini mtoto kaenda
shule kumbe anafanyiwa ufedhuli wa aina hiyo,” alisema.
Aliwataka wazazi kujenga utamaduni wa
kuwachunguza watoto wao mara kwa mara kila wanaporudi kutoka shuleni ili
kubaini kama kuna mabadiliko ya kitabia au kutokuwapo shuleni kwa kipindi
fulani. Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Jeshi Lupembe aliahidi kwenda katika
shule hiyo leo kuchunguza suala hilo.
Tukio hilo linafanana kwa kiasi na lile la
mwanamuziki, Nguza Viking “Babu Seya” na mwanaye, Johnson Nguza “Papii Kocha”
wanaotumikia kifungo cha maisha jela baada ya kutiwa hatiani.
Wanamuziki hao, walihukumiwa mwaka 2004 baada ya
kupatikana na hatia ya kubaka na kunajisi watoto 10 wenye umri wa kati ya miaka
sita na minane wa Shule ya Msingi Mashujaa, Dar es Salaam na sasa wamekata
hukumu katika Mahakama ya Afrika Mashariki kupinga hukumu hiyo.
No comments:
Post a Comment